WATANZANIA WAASWA KUTUMIA MPANGO WA FEDHA ILI KUJILETEA MAENDELEO

Na Immaculate Makilika na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Serikali yawataka watanzania kutumia  Mpango Mkuu wa Maendeleo wa  Sekta ya Fedha ya mwaka 2020/21 hadi 2029/30 ili kujiletea maendeleo kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi.



Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mpango huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga  kwa  niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Doto James alisema kuwa  lengo la kuandaa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ni kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wote zikiwemo huduma za bima, mikopo, akiba, uwekezaji na kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na sekta ya viwanda.

“Wananchi na watanzania wote kwa ujumla, nitoe wito wa kutambua na kujinufaisha na Mpango huu katika kujiletea maendeleo yenu katika ngazi mbalimbali. Utatuzi wa changamoto zilizokuwepo unatoa fursa kubwa na pana zaidi ya kujikwamua kiuchumi kwa kupata mitaji, huduma za benki, bima na nyinginezo kwa unafuu na ufanisi zaidi”, alisema Maganga.

Aidha, aliongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.  

Naibu Katibu Mkuu huyo  alifafanua kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ni kujenga msingi wa uchumi wa viwanda, kuimarisha jitihada za kukuza uchumi na kuondoa umaskini wa kipato. Aidha, uimara wa sekta ya fedha ndiyo nyenzo muhimu ya ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda.

Aliongeza kuwa maboresho yaliyofanyika katika sekta ya fedha yameleta matokeo chanya ambapo hadi kufikia Desemba 2019 kumekua na ongezeko la idadi ya benki na taasisi za fedha  kutoka 10 hadi 60, kampuni za bima kutoka mbili hadi 32, kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam kufikia 28, kuanzishwa kwa mifuko ya uwekezaji wa pamoja na kufikia tisa, Taasisi za huduma ndogo za fedha kufikia 450 na Vyama vya Ushirika vya kuweka na kukopa kuongezeka hadi 4,770 Tanzania Bara na 231 Tanzania visiwani.

“Vyuo Vikuu, Taasisi mbalimbali za Elimu ya Juu pamoja na Taasisi za Utafiti; ni matumaini yangu kwamba kupitia Mpango huu mtaziona fursa mbalimbali zilizomo na kujipanga katika kuboresha maeneo mbalimbali ya kitaaluma na kiutafiti ili kuhakikisha sekta hii inaendelea kuwa juu, ya kisasa, yenye ushindani na kuweza kuhimili mabadiliko ya nyakati kwa wepesi na weledi mkubwa”, alisisitiza Maganga.

Naye, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya Kati (TIRA), Stella Rutabuza alisema kuwa mpango huo utaondoa changamoto nyingi ambazo wasimamizi wa Bima wanakutana nazo.

“Mpango huu umetoa mapendekezo na mikakati ambayo itasaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za bima kwa katika maeneo mbalimbali hasa ya vijijini na maeneo ya mjini ambayo wananchi hawana uelewa kuhusu bima”, alisema Rutabuza.
Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527