DHANA POTOFU DHIDI YA WALEMAVU YAANZA KUTOWEKA

Na Abby Nkungu, Singida
DHANA potofu  iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya wazazi na walezi  Manispaa ya Singida kuwa  watoto  wenye  ulemavu hawastahili wala hawana haki ya  kupata elimu ya awali imepungua, kufuatia kundi hilo kuanza kuandikishwa na kusoma kama ilivyo kwa  wengine.

Awali, ilielezwa kuwa kukithiri kwa imani potofu miongoni mwa baadhi ya wananchi ni moja ya sababu ya watoto wengi wenye ulemavu wa aina mbalimbali kutokupata elimu ya awali kutokana na kufichwa nyumbani bila kwenda kuandikishwa shuleni hadi wanapokuwa wakubwa kupindukia.

Hali hiyo, ilidaiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya watoto hao kitaaluma kiasi cha kufanya vibaya kwenye masomo yao ya kila siku darasani na mitihani ya kitaifa mwaka hadi mwaka.
Hata hivyo, Mwalimu Mkuu wa  shule ya Msingi Tumaini Viziwi ya Mjini Singida, Francis Edward baada ya kutumia  viongozi wa Serikali za mitaa,  dini,  mila, watu  maarufu na  vyombo vya habari kupinga dhana hiyo potofu, sasa watoto hao wameanza kuandikishwa shule wakiwa na umri unaostahili.
“Tangu kuanzishwa kwa shule hii ya Viziwi miaka 18 iliyopita, tulikuwa hatujawahi kupata  wanafunzi wa awali lakini baada ya nyie waandishi wa habari kuja na kuandika kwenye vyombo vyenu, dhana hii iliyoota mizizi imeanza kupungua na kwa mara ya kwanza  tumeandikisha watoto watano” alisema.
Alifafanua kuwa  watoto hao  watano; wakiwemo wavulana  wanne na msichana mmoja,  ni idadi ya kutosha kwa mujibu wa Sera ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum ambapo  idadi darasani  inatakiwa kuwa kati ya wanafunzi 5 hadi  10  ili  kuweza kuwahudumia vyema kitaaluma.
Mwalimu Edward alieleza kuwa kuandikishwa kwa watoto wenye ulemavu katika shule za Awali kutawajengea uwezo wa kufanya vizuri kwenye masomo yao pindi wanapoingia darasa la Kwanza tofauti na hapo mwanzo ambapo watoto hao walikuwa wanaandikishwa wakiwa na umri kati ya miaka 10 na 15.
“Hapo kabla, watoto hawa walikuwa wanafichwa majumbani hadi wanapogundulika baadae  sana wakiwa  wakubwa na kuletwa hapa shuleni wakiwa na miaka zaidi ya 10. Hatukuwa na namna zaidi ya kuwapeleka darasa la Kwanza moja kwa moja; hivyo kuwavusha darasa la Awali” alifafanua.
Alisema kuwa hali hiyo ilikuwa inawaathiri kielimu watoto hao kwa kuwa walikosa msingi muhimu ambao hutolewa katika shule za awali ili kumjenga mtoto kiakili na kimwili katika kupokea masomo yake ya madarasa ya juu.
Baadhi ya wananchi wameshauri kuwa  njia pekee ya kumaliza changamoto hiyo ni  kwa  wadau  kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto wenye ulemavu badala ya kuwaficha nyumbani lakini pia kuwashirikisha wanasiasa katika jambo hilo. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527