MILIONI 410 KUTUMIKA KUKARABATI SKIMU ZA UMWAGILIAJI IRINGA NA KILOLO


Serikali itatoa shilingi milioni 410 kwa ajili ya kukarabati skimu za umwagiliaji mashamba yaliyoharibiwa na mafuriko mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na mto Ruaha kuacha njia yake ya asili.


Kauli hiyo imetolewa jana (04.09.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipofanya ziara ya kukagua uharibifu wa skimu za umwagiliaji za Pawaga na Ruaha Mbuyuni mkoani Iringa.

Kusaya amezitaja skimu ambazo zitanufaika na fedha hizo kuwa ni Mkombozi,  Mlenge, Luganga na Magozi wilaya ya Iringa zitakazopewa shilingi milioni 350 na skimu ya umwagiliaji Ruaha Mbuyuni itapewa shilingi milioni 60.

“Imenisukuma kuja hapa Pawaga kuona hali halisi ya uharibifu wa skimu zetu 4 za umwagiliaji zilizoharibiwa na mafuriko na kuwa Wizara ya Kilimo italeta shilingi milioni 350 mapema wiki ijayo ili kukarabati miundombinu “alisema Kusaya

Akiwa katika skimu ya Mkombozi , Mlenge, Magozi na Luganga wilaya ya Iringa Katibu Mkuu huyo alisema atatuma wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji pamoja na mitambo (greda) kurekebisha miundombuni hiyo iliyoharibiwa kufuatia mto Ruaha mdogo kuacha njia yake ya asili.

“ Nahitaji jumatatu tarehe 07.09.2020 mitambo iwepo hapa Pawaga na wataalam ili kazi ya kurejesha mto ianze na wakulima wapate maji kwenye mashamba yao” alisema Kusaya.

Kusaya aliwaambia wakulima wa mpunga kwenye skimu hizo kuwa serikali ya awamu ya tano ipo bega kwa bega kuhakikisha skimu za umwagiliaji zinakuwa bora na kufanya kazi mwaka mzima,hivyo wakulima watoe ushirikiano kwa Tume kufanikisha ukarabati wa skimu.

Aliwahakikishia wakulima wa mpunga kwenye skimu hizo kuwa hakuna atakayechangishwa fedha  bali serikali ndio itatoa fedha hizo kukarabati miundombinu ya umwagiliaji iliyoharibika na kuwa  jukumu la wananchi ni kushirikiana na wataalam kwa kazi ndogo ndogo kama kubeba mawe na mchanga  kwenye maeneo ya kazi.

“ Nataka ndani ya wiki moja kuanzia sasa wataalam wa Tume ya Umwagiliaji mfanye kazi ya kuurejesha mto Ruaha mdogo kwenye njia yake ,vifaa na mitambo ipo .Wakulima wanachohitaji ni maji yafike kwenye mashamba yao haraka” aliagiza Kusaya

Akiwa katika skimu ya umwagiliaji Ruaha Mbuyuni Katibu Mkuu Kusaya alijionea jinsi mto Ruaha ulivyoacha njia zaidi ya mita 100 na kufanya banio kutokupitisha maji na wakulima kushindwa kulima zaidi ya hekta 450 msimu huu.

Aliwahakikishia wakulima hao kuwa Wizara ya Kilimo itafanya kazi ya kurejesha mto kwenye njia yake ya asili ili maji yafike kwenye mashamba ya wakulima kwa kuwa mto huo ndio tegemeo la wakulima kuzalisha mazao ya chakula yakiwemo mpunga,mahindi na mazao ya mboga mboga (horticulture).

Kusaya ameahidi kuwa baada ya wiki mbili atarudi wilaya za Kilolo na Iringa kukagua maendeleo ya kazi ya kurejesha mto kwenye njia yake na kuwa amezitaka halmashauri hizo kushirikiana na Wizara  kukarabati miundombinu hiyo mapema.

Akizungumza kwenye ziara hiyo mkulima Fundi Mihayo wa kijiji cha Luganga wilaya ya Iringa aliishukuru Serikali kwa kuguswa na matatizo ya wakulima na kuchukua hatua.

Alisema katika mvua nyingi zilizonyesha mwezi Januari mwaka huu zilisababisha mafuriko yaliyoharibu skimu hivyo kusababisha mazao kuharibika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bashiri Mhoja alisema mwaka huu wakulima walipata hasara kwa kuzalisha asilimia 2 tu ya zao la mpunga kutokana na miundombinu ya skimu za umwagiliaji  kuharibiwa na mafuriko hivyo ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa hatua ya kutoa fedha na wataalam  kukarabati.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ruaha Mbuyni wilaya ya Kilolo Hamis Matabazi alisema wanakijiji wapo tayari kutoa ushirikiano kwa serikali kufanikisha urejeshaji mto Ruaha mdogo kwenye njia yake kwani wana uhitaji mkubwa wa kuendelea na kazi ya uzalishaji mazao.

“ Tunaomba Katibu Mkuu utufikishie salamu zetu kwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa kusikiliza kilio chetu wananchi wa Ruaha Mbuyuni na kuleta fedha za kukarabati skimu yetu hii” alishukuru mwenyekiti wa kijiji chicho .

Katibu Mkuu Kusaya pia alitoa wito kwa wakulima wa Kilolo na Iringa kutunza mazingira kwa kupanda miti kandokando ya mto Ruaha ili kulinda kingo  za mto zisiharibiwe na mvua.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post