CHADEMA WAZINDUA KWA KISHINDO KAMPENI TARIME VIJIJINI... HECHE ATEMA CHECHE


 Mgombea Ubunge jimbo la Tarime vijijini kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika uwanja wa Tarafa Sirari.
*****

Na Mwandishi wa Malunde 1 blog Tarime

Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Vijijini John Heche kupitia chama cha Democrasia na Maendeleo(CHADEMA)amezindua rasmi kampeni zake na kueleza mambo mbalimbali aliyoyatekeleza wakati akiwa mbunge huku akiwaomba wananchi kumchagua tena ili aendelee kuleta maendeleo.

Heche aliyasema hayo jana wakati CHADEMA wakizindua kampeni za uchaguzi jimbo la Tarime Vijijini katika uwanja wa Tarafa kijiji cha Sirari kata ya Sirari wilayalani Tarime,uzinduzi ambao uliohudhuriwa na viongozi wa chama hicho kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Mara,wakiwemo wagombea Ubunge kupitia chama hicho pamoja na Wananchi.

Heche alisema kuwa iwapo kura hazitatosha atawashukuru wananchi na kwenda kufanya shughuli zake kwa sababu anaamini katika demokrasia vinginevyo atahakikisha anapambana ili haki ipatikane huku akiwaomba wananchi wamchague pamoja na Mgombea urais Tundu Lissu na madiwani wa CHADEMA.

Akizungumzia maendeleo yaliyofanyika Heche alisema kuwa miradi mbalimbali imetekelezwa katika awamu yake ya ubunge,ikiwemo miradi mbalimbali ya ujenzi wa Zahanati,Vituo vya Afya,HospitalI ya Halmashauri,Miundobinu ya Barabara,mikopo, na miradi mingineyo.

Aliongeza kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo ni kutokana na halmashauri hiyo kuongozwa na CHADEMA ambapo Madiwani walisimamia miradi vizuri na masuala mbalimbali ya maendeleo.

Baadhi ya wagombea ubunge kutoka majimbo mbalimbali mkoani Mara nao wakampigia kampeni mgombea huyo na kuwataka wananchi wampigie kura Heche,Tundu Lissu kwa upande wa Urais na madiwani wa CHADEMA.

Mgombea Ubunge jimbo la Bunda mjini Esther Bulaya kupitia chama hicho aliwaomba wananchi kumchagua Heche kwani ndiyo anazijua shida za Tarime hivyo atatatua kero za wananchi.

Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime mjini Esther Matiko alisema Heche ni kiongozi mzuri hivyo kuwaomba wananchi wampe kura.

Mgombea Ubunge jimbo la Serengeti  Catherine Luge alisema kuwa amefanya kazi na John Heche anamfahamu katika utendaji wake wa kazi na amekuwa akitetea haki ya maslahi ya wananchi wa Tarime.

"Chadema imetoa wanawake watatu kutoka Mara kugombea ubunge sisi ni wasubhati (Mabinti)zenu tupeni kura mpeni John ili akamilishe mipango iliyosalia kwa maendeleo ya Tarime", alisema Luge.

Mgombea Ubunge jimbo la Musoma mjini Mwita Julius aliwaomba wananchi kuipigia kura Chadema kwa kuwa ni chama kinachotetea matatizo ya wananchi.

Mgombea Ubunge kutoka jimbo la Rorya Ezekiel Wenje alisema kuwa Heche ni mtu mwenye msimamo na amekuwa akifanya kazi nzuri akiwa bungeni na kwamba majimbo ya Tarime yamekuwa kimaendeleo ikilinganishwa na jimbo la Rorya.

Mzee maarufu kutoka kijiji cha Bisarwi kata ya Manga Marwa Kisang'ore alisema:
"Heche ni mfuata nyayo mzuri Apiri,2,2017 tulifukuzwa kwenye ardhi  kuanzia huko Nyamongo,Nyawana,Weigita,Kiore,hadi kirumi Heche alitupigania na Serikali ikazuia ardhi yetu kuporwa,alitusemea bungeni na ardhi ikarudi mikononi mwetu kura zote tutampa Heche".

Katibu wa CHADEMA wilaya ya Tarime Hamis Nyanswi alisema"kuna watu wanaona Chadema imepoteza mwelekeo sisi hatujapoteza mwelekeo tuna sababu ya kuichagua Chadema kwa kuwa ni mwakilishi wa wananchi, watu wanasema ukiichagua Chadema maendeleo hayaji mbona Rorya haina maendeleo ikilinganishwa na majimbo ya upinzani japo imeongozwa na CCM ".

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mara Lucus Ngoto alisema kuwa katika kuhakikisha wanawake wanapata nafasi za uongozi kimeteua wanawake 3 kati ya majimbo 10 kugombea ubunge wa jimbo.
 Mgombea Ubunge jimbo la Tarime vijijini kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika uwanja wa Tarafa Sirari.

 Mgombea Ubunge jimbo la Tarime vijijini kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwatubia wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika uwanja wa Tarafa Sirari.
 Mgombea ubunge jimbo la Tarime kupitia chama  cha Democrasia na Maendeleo CHADEMA Esther Matiko akimnadi mgombea ubunge jimbo la Tarime vijijini John Heche wakati wa uzinduzi wa kampeni za Heche
Wagombea ubunge majimbo ya mkoa wa Mara kupitia CHADEMA wakiwa wenye uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime vijijini John Heche
 
Mgombea ubunge jimbo la Bunda mjini kupitia CHADEMA Esther  Bulaya akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime vijiji John Heche.
 Wafuasi wa CHADEMA na wananchi wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime vijijini John Heche.
 Wagombea ubunge na wafuasi wa CHADEMA wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za John Heche mgombea ubunge jimbo la Tarime vijijini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527