DKT.CHAULA ALITAKA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA KUJIIMARISHA ZAIDI UTOAJI WA HUDUMA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta ya Mawasiliano, Dk.Zainabu Chaula,   amewataka  watumishi wa shirika la posta Tanzania  kuwajibika katika utendaji kazi  ili kuleta chachu ya mabadiliko katika shirika hilo.

Dkt.Chaula amebainisha hayo jijini Dodoma  wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa Shirika la Posta Tanzania ambapo amesema ni wajibu kwa kila meneja wa Shirika la Posta kuweka malengo ya makusanyo na kuongeza wigo ili kujitangaza zaidi kwa huduma zinazotolewa na shirika hilo.

“Nyie mnajukumu la usafirishaji vitu mbalimbali vya taasisi za umma kwa mfano Wizara ya Afya inawatumia kusafirisha sampuli za damu, sampuli za vitu vingi hadi maabara ya Taifa, “amesema.

Amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa bidii ili kupata matokeo mazuri katika kuhudumia jamii na kupata fursa kiuchumi.

“Lazima katika kipindi cha miaka mitano ijayo tufike uchumi wa juu, lakini tutafikaje kama hatuna uwajibikaji wa pamoja wa matokeo, tupo Tanzania ya kidigitali, tunatumia mifumo, anuani za makazi, posta kiganjani hakuna haja ya kukimbizana na daladala, tuma mzigo kwa njia ya posta na utafikishiwa hadi nyumbani wakati unafanya kazi nyingine,”amesema.

Dk.Chaula amelitaka shirika hilo kujiimarisha zaidi kwenye utoaji huduma na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya kwanza barani Afrika na ulimwenguni kwa utoaji huduma.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mang’ombe alisema mafunzo hayo yamewakusanya mameneja wa shirika hilo wa mikoa yote nchini ili kuweka mikakati juu ya kuongoza shirika kwa pamoja.

“Tunatengeneza kitu cha maelewano ya pamoja, kwanini sisi ni viongozi, kitu gani tufanye ili twende mbele, tumekusanyika hapa ili kuangalia majukumu yetu ya kila siku, kila mtu apate kupangiwa majukumu na kuyasimamia ili kupata matokeo chanya,”amesema.

Amesema shirika hilo lina majukumu mbalimbali ya kuwahudumia wananchi, ikiwemo barua, usafirishaji wa nyaraka muhimu(EMS), kaunta na Wakala na kuna taasisi zaidi ya 350 ambazo zinatumia huduma ya posta huku watanzania asilimia 50 wanatumia huduma hizo.

“Posta imejiandaa kiutendaji kazi, Posta ndio tulikuwa wasafirishaji wakubwa wa sampuli za Corona na tumefanya kwa asilimia 100, tulipeleka Dar es salaam ndani ya saa 24,”amesema.

Ameeleza kuwa tayari wamejipanga kwa kuwa na wafanyakazi na pikipiki za kutosha ili  kusafirisha sampuli ambapo ilianza kazi hiyo tangu mwaka 2012.

“Tunafanya kazi kila siku, kadri soko linavyopanuka na sisi tupo tayari kuwahudumia watanzania,tunataka Tanzania iwe kama kijiji, ukienda kwenye mifumo ya posta, unafungua maduka mbalimbali na kununua bidhaa yeyote,”amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post