TCRA YAWATAKA WATOA HUDUMA YA HABARI MTANDAONI 'BLOGGERS' KUANDIKA HABARI SAHIHI


Mkurugenzi wa Leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) Mhandisi Andrew Kisaka akizungumza kwenye Mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni ‘Online Content Service Providers’ uliolenga kujadili masuala mbalimbali ya mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2020 leo Jumanne Septemba 15,2020
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles akizungumza mbele ya Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni (hawapo pichani),wakati akifungua Mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni,uliofanyika leo katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es salaam.
**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka watoa huduma ya habari mtandaoni kuhakikisha waandika habari sahihi na bila kuegemea upande wowote hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2020.

Mhandisi Kisaka ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 15,2020 wakati akitoa mada kuhusu Kanuni za Utangazaji wakati wa uchaguzi za mwaka 2015 kwenye Mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni ‘Online Content Service Providers’ uliofanyika katika kituo cha mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam. 

 "Muwe makini mnapoandika habari, usiegemee upande mmoja.
Unaporipoti hakikisha hujaongeza mtazamo wako,usiongeze ongeze maneno yako. Hakikisha unawapa nafasi sawa wagombea wote wa vyama vya siasa",alisema Mhandisi Kisaka. 

"Usitoe nafasi kwa mgombea anayetumia lugha kali na chafu inayoweza kuhatarisha amani ya nchi. Kamwe chombo chako cha habari kisitumike kuhamasisha au kuonesha kitu cha hovyo. Ukiona kitu cha hovyo unaweza kukatisha matangazo",aliongeza Mhandisi Kisaka.

Akifungua Mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Charles amewataka Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni kuvipa nafasi sawa vyama vyote vya siasa na kuepuka kuandika habari zenye kuhamasisha vurugu na kusababisha uvunjivu wa amani. 

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi tunavipongeza vyombo vya habari mtandaoni kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkitupatia. Tumewaita ili kuwajengea uelewa kuhusu mkachato wa uchaguzi,tunaamini kuwa mna nafasi kubwa ya kuelimisha jamii kuhusu taratibu mbalimbali za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenda kupiga kura Oktoba 28,2020”,amesema Dkt. Charles. 

Mkutano huo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Watoa huduma ya habari Mtandaoni wanaoendesha Blogu na Runinga za mtandaoni uliolenga kujadili masuala mbalimbali ya mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2020  ili kuwajengea uwezo watoa huduma ya habari mtandaoni kuhusu masuala ya uchaguzi ili waweze kuandika habari kwa usahihi na kulinda amani ya nchi. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post