WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ASHIRIKI MAZIKO YA MTUMISHI WA OFISI YA WAZIRI MKUU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo (Jumatano, Agosti 5, 2020) ameshiriki maziko ya aliyekuwa mtumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu marehemu Bw. Joseph Ndonjekwa yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu Bunju Mabwepande jijini Dar es Salaam.


Bw. Ndonjekwa ambaye alihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2006  akitokea Ofisi ya Rais amefariki dunia Agosti 2 mwaka huu katika Hospitali ya Emilio Mzena Memorial (EMMH) ambako alikuwa amelazwa baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Waziri Mkuu  amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mtumishi mwenzao aliyefanya kazi yake kwa weledi na uadilifu mkubwa, hivyo amesisitiza kwa  mke wa marehemu, familia na watumishi wa Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu waendelee kuwa watulivu na waendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema.

“Msiba huu umetugusa sana sisi  ndio tulikuwa tunafanyanaye kazi kwani aliajiriwa na Ofisi ya Rais na alipangiwa Ofisi ya Waziri Mkuu kama kituo chake cha kazi tangu mwaka 2006 na amekuwa dereva wa Waziri Mkuu kuanzia Mhe. Fredrick Sumaye, Mhe. Edward Lowasa, Mhe. Mizengo Pinda."

Waziri Mkuu ameongeza kuwa "Maisha yangu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, maeneo yote na wilaya zote nilizotembelea yeye ndiye alikuwa ananiendesha. Tulienda salama na kurudi salama ni kwa sababu ya umakini na weledi wake mkubwa wa kufanya kazi."

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bw. Diwani Athumani amesema ni majonzi makubwa kwa Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kufuatia msiba huo. "Wote tukumbuke kuwa hii ni safari ya kila mmoja tunapishana kwa wakati na haya ni maamuzi ya Mwenyezi Mungu tunatakiwa tumuombee roho yake ilazwe mahala pema."

Marehemu Bw. Joseph Ndonjekwa alizaliwa Aprili 30, 1962 katika wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya na alipata elimu ya msingi kwenye shule ya msingi Mjimwema wilayani Ilala jijini Dar es Salaam kuanzia mwaka 1971 hadi 1977 na mwaka 1978 hadi 1979 alipata na elimu ya watu wazima. Aliajiriwa katika Ofisi ya Rais Septemba 1, 1979.

Maziko hayo pia yamehudhuriwa na Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Godfrey Chongolo pamoja na watumishi wa Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu.


(Mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 5, 2020.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post