Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MVUA KUBWA YASABABISHA MAFURIKO MAGEUZI, SHINYANGA

Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog

Wakazi wa Mtaa wa Mageuzi, Kata ya Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga wameingiwa na hofu baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji ya mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa takribani saa moja na kusababisha maji kujaa katika maeneo ya makazi.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema mvua hiyo kubwa iliyonyesha Machi 10,2026 imesababisha maji kukosa muelekeo na hatimaye kuingia ndani ya makazi ya wananchi, hali iliyozua taharuki na hofu ya kuharibika kwa mali pamoja na usalama wa wakazi wa eneo hilo.

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mageuzi wameeleza kuwa chanzo kikubwa cha tatizo hilo ni ukosefu wa miundombinu ya mitaro ya kupitisha maji pembeni mwa barabara, jambo linalosababisha maji ya mvua kukosa njia sahihi ya kupita.

Aidha, wakazi hao wamedai kuwa shughuli za kilimo cha mpunga zinazofanywa na baadhi ya wananchi ndani ya mkondo wa mto zimekuwa zikichangia kuziba njia ya asili ya maji, hali inayosababisha maji kujaa na hatimaye kuingia katika makazi ya watu.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, Bi. Asha Raphael, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa ni tatizo linalohitaji ufumbuzi wa haraka ili kuzuia madhara makubwa zaidi kwa wananchi.

“Ni kweli baadhi ya nyumba zimezingirwa na maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha. Tunaomba mamlaka husika iingilie kati kwa kuweka miundombinu bora ya mitaro ya maji ili kuondoa tatizo hili,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mageuzi, Bw. Vitalis Mugisha, amesema tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa miundombinu madhubuti ya kupitisha maji pamoja na shughuli za kilimo zinazofanyika ndani ya mkondo wa mto.

Amesema hali hiyo imefanya maji ya mvua kukosa mwelekeo sahihi na hatimaye kuingia katika makazi ya wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia madhara zaidi wakati huu wa msimu wa mvua unaoendelea.

Wakazi wa eneo hilo wameiomba Serikali pamoja na mamlaka za Manispaa ya Shinyanga kuchukua hatua za dharura, ikiwemo ujenzi wa mitaro ya maji na kudhibiti shughuli za kilimo ndani ya mikondo ya mito ili kuondoa hatari ya mafuriko inayoweza kuhatarisha maisha na mali za wananchi.

















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com