WAZIRI KILIMO AZINDUA MFUMO WA KUHAKIKI MBEGU NA PEMBEJEO, 'T-HAKIKI'


Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akizindua rasmi huduma maalum ya kuhakiki pembejeo inayofahamika kwa jina la 'T-hakiki' ndani ya Banda la Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL), kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nyakabindi Mkoa wa Simiyu. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Patrick Ngwediagi (kushoto) wakishiriki tukio hilo.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Patrick Ngwediagi (kushoto) wakipiga makofi mara baada ya uzinduzi huo.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma maalum ya kuhakiki pembejeo inayofahamika kwa jina la 'T-hakiki' ndani ya Banda la Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL), kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nyakabindi Mkoa wa Simiyu. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba akizungumza kwenye uzinduzi huo wa huduma maalum ya kuhakiki pembejeo inayofahamika kwa jina la 'T-Hakiki', uliofanyika ndani ya Banda la Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL), kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nyakabindi Mkoa wa Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel akizungumza katika uzinduzi huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Patrick Ngwediagi (kushoto) akizungumza katika uzinduzi huo.
****
Na Mwandishi Wetu, Simiyu
WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga amezindua rasmi huduma maalum ya kuhakiki pembejeo inayofahamika kwa jina la 'T-hakiki'.

T-Hakiki ni mfumo wa njia ya simu ambapo unabofya *148*52# na kuingiza namba zilizo kwenye sehemu yenye kivuli kwenye vifungashio vya mbegu au kwenye chupa za viuatilifu ili kuthibitisha uhalisia wa pembejeo.

Uzinduzi wa huduma hiyo inayolenga kuwakomboa wakulima katika mapambano dhidi ya mbegu na viuatilifu feki, umefanyika jana ndani ya Banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nyakabindi mkoania Simiyu.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Hasunga alisema uuzaji wa pembejeo feki za kilimo umesababisha athari kubwa kijamii na kiuchumi.

“Matokeo yake yamesababisha changamoto nyingi kwa sekta ya kilimo ambayo ndiyo sekta muhimu inayochangia kuongeza tija kwenye uchumi wa Taifa, kwa maana hiyo huduma hii ni mkombozi halisi kwa wakulima wetu.

Alisema huduma hiyo imetokana na ubunifu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kwa kushirikiana na Kampuni ya Quincewood Group Limited na wadau wa sekta ya kilimo kama vile Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) na Taasisi ya Utafiti  na Udhibiti wa Viuatilifu (TPRI), ambao sasa wamekuja na suluhisho la kiteklonojia kukomesha matumizi ya pembejeo feki.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel alisema ubunifu huo umeenda sambamba na malengo ya Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo.

Wakati Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Patrick Ngwediagi  alisema huduma hii itamsaidia mkulima kufahamu matumizi sahihi ya pembejeo hizo kupitia simu ya mkononi, hakika haya ni mapinduzi bora ambayo yatazidi kumkomboa mkulima lakini pia kuisaidia Serikali kukabiliana na wafanyabiashara wa pembejeo wasio waadilifu.

"T-Hakiki itaboresha sekta ya kilimo na italinda maisha ya wakulima wengi katika kuendesha shughuli za kilimo na kulinda thamani ya fedha zao," alisema.

JINSI T-HAKIKI INAVYOFANYA KAZI!
Aidha, akifafanua namna mfumo huo unavyofanya kazi, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba  alisema T- Hakiki ni huduma ya simu ya mkononi ambayo ni mkombozi kwa sekta ya kilimo nchini, pia inalinda maisha ya wakulima wengi kwa kuongeza  usalama wa chakula nchini Tanzania.

Alisema teknolojia hiyo inakusudia kufungua ukurasa mpya kwa wakulima kwa kuja na suluhisho ambalo linapatikana kirahisi. Kwa sababu huduma hii itawasaidia wakulima kutambua pembejeo feki na kuzitolea taarifa kama hatua mojawapo ya kukomesha matumizi ya pembejeo feki.

“T-Hakiki ni mfumo wa njia ya simu ambapo unabofya *148*52# na kuingiza namba za siri zilizo kwenye vifungashio vya mbegu au kwenye chupa za viuatilifu ili kuthibitisha uhalisia wa pembejeo. Huduma ya T-Hakiki inapatikana katika mitandao yote ya simu na ni bure,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527