RC KUNENGE AIPONGEZA JUMUIYA YA KHOJA SHIA ITHNASHERI KWA KUFANIKISHA ZOEZI LA UCHANGIAJI DAMU


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri, Dk. Shaneabbas Jaffer wakati wa zoezi la uchangiaji damu lililofanyika katika Hospitali ya Ebrahim Haji kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
Sheikh Sayed Idairous kutoka katika Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri akitoa maelezo wakati wa zoezi la uchangiaji damu lililoendeshwa na Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Hospitali ya Ebrahim Haji
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri, Azim Dewji akitoa maelezo wakati wa zoezi la uchangiaji damu lililoendeshwa na Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Hospitali ya Ebrahim Haji
 ***
Dar es Salaam, Tanzania, Jumapili 23/08/2020 – Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Abubakar Kunenge ameipongeza Jumuiya ya Khoja Shia kupitia programu yake ya “Husayni Blood Drive” kwa kufanikisha zoezi la uchangiaji damu kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Hospitali ya Ebrahim Haji. Zoezi hilo la uchangiaji damu limefanyika katika Hospitali ya Ebrahim Haji iliyopo jijini Dar es Sala ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbumbuku ya kifo cha mjukuu wa Mtume Muhammed (SAWW), Imam Hussain lakini pia ikiwa ni kuendeleza utamaduni wa kujitolea kwa jamii ambao ni msingi mkuu wa ujumbe wa Imam Hussain.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa amepongeza jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kwa tukio hilo lenye upendo kwa kuwa linaenda kuokoa maisha ya watu. “Nimeambiwa kuwa zoezi hili limefanyika kwa zaidi ya miaka 15 na kukusanya zaidi ya lita 5000 za damu ambazo zimesaidia kuokoa maisha ya watanzania wengi jambo ambalo ni lenye upendo mwingi kwani watu hawa wanachangia damu bila kujali inakwenda kumsaidia nani” alisema Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa amesema watu wengi wanapenda kutoa msaada pale ambapo wana uhakika wa kupata shukrani na hivo kutoa msaada kwa watu wanaowajua au kuwaona lakini Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri imefanya sadaka iliyobora kwa kutoa damu kwa watu wasiowajua ambao hawatopata hata nafasi ya kuwashukuru na hiyo ndiyo sadaka bora kwa mujibu wa vitabu vya dini. Mkuu wa Mkoa pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri, Azim Dewji kwa kushiriki katika matukio mengi ya kitaifa ikiwemo kutoa nyumba yake binafsi ili kutumika kama kituo cha kuhudumia wagonjwa waliopata maambukizi ya Corona.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri, Azim Dewji alisema kuwa jumuiya hiyo imekua ikishiriki katika mambo mengi ya kijamii ambapo mapema mwaka huu, Jumuiya hiyo hiyo ilitumia siku 45 kujenga wodi mpya yenye vitanda 60 katika Hospitali ya Ebrahim Haji ili kusaidia wagonjwa waliopata maambuzi ya Corona. Hata hivo kutokana na kupungua kwa maambukizi ya Corona nchini, wodi hiyo sasa itatumika kuhudumia akina mama na watoto. Pamoja na hilo kila Jumamosi hospitali hiyo hutoa huduma bure za matibabu kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii.

Nae Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu Kanda ya Mashariki, Judith Goshashy ameipongeza Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kwa kuwa wachangiaji wazuri wa damu kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) tangu walipoanza kushirikiana nao mnamo mwaka 2008. “Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita tumekua tukipokea wastani wa wachangiaji damu 440 kila mwaka kutoka katika Jumuiya hii jambo ambalo ni la kupongezwa sana ukizingatia huwa wanajitolea damu mara 2 kwa mwaka”, alisema Judith. 

Sheikh Sayed Idairous ambae ni mmoja wa viongozi wa dini kutoka katika Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri, alisema kuwa wajibu wa viongozi wa dini katika nchi ni kujenga undugu bila kujali itikadi za dini wala kabila na hivyo wao wamechagua kufanya zoezi hilo la uchangiaji damu ambalo linakwenda kusaidia watu bila kujali itikadi zao. “ Damu hii inayotolewa hapa haitouliza dini ya mtu wala kabila lake bali itakwenda kusaidia kukoa maisha ya watu na huo ndio wajibu wetu” alisema Sheikh Sayed.
Pamoja na zoezi la kuchangia damu,Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri pia hushiriki katika shughuli nyingine za kijamii ikiwemo utoaji wa maji safi, uchunguzi na upasuaji wa mtoto wa jicho, uchunguzi wa saratani zinazoathiri wanawake ikiwemo saratani ya matiti na mlango wa kizazi. “Huduma hizi zimekua zikifanyika kwa takribani miaka 5 sasa na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote wanaojitokeza” alisema Dr. Alihussein Molloo ambae ni mwanajumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri na Mkurugenzi wa Hospitali ya Ebrahim Haji.


Kwa maelezo zaidi:
Jina
Mawasiliano
Dr. Alihussein Molloo
0689400300




Ashura Blood Donation Statistics



Last 6 Years




Male
Female
Total
2014
209
84
293
2015
233
103
336
2016
302
122
424
2017
282
148
430
2018
302
164
466
2019
304
124
428
Total Donations in 6 Years
1632
745
2377









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527