SPRF YAWAKUTANISHA WADAU WA MASUALA YA KISHERIA KUJADILI MATUKIO YA UKATILI KUPITIA MRADI WA 'AWARE 2020'


Mkurugenzi Mtendaji wa  Shirika  la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) nchini, Dkt.Suleiman Muttani, akizungumza kwenye kikao kilicho wakutanisha wadau mbalimbali  wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kujadili matukio ya ukatili wa kijinsia.


Baadhi ya wadau wakiwa kwenye kikao hicho.

Wadau wakiwa kwenye kikao hicho.
Mratibu wa Field wa Shirika hilo, Bernard Maira, akizungumza.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ikungi, Haroun Yunus Haroun akizungumzia  mfumo wa mawasiliano wakupeana habari za matukio ya ukatili wa kijinsia.


Mshauri wa Masuala ya Sheria  wa  SPRF na  Mratibu wa mradi huo Msaidizi, Paul Kigeja akitoa mada kuhusu haki ya mwanamke na mtoto.


Michango ya taarifa ikitolewa.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Damankia William Hangida akichangia janbo.


Malietha Kibao akichangia janbo.

Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Mwedinuu Beleko, akitoa takwimu za matukio ya ukatiki. 

Mada zikitolewa.

Dalahile Mahende wa Dawati la Jinsia, akizungumziz kesi mbalimbali.
Afisa Upelelezi kutoka Kituo cha Polisi cha wilaya hiyo, Athumani Makoba, akizungumzia jinsi wanavyoshughulikia kesi za ukatili.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Ikungi, Lutengano Kabigi, akizungumzia nini kifanyike ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo  Wilaya ya Ikungi,  George Francis, akizungumzia jinsi wanavyoshughulikia kesi za ukatili.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo ya Kata ya Mungaa,  Frida Shaidi, akizungumzia jinsi wanavyoshughulikia kesi za ukatili.


 Picha ya pamoja


Na Dotto Mwaibale, Singida 
SHIRIKA  la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) kupitia mradi wa ‘AWARE 2020’limewakutanisha wadau mbalimbali  wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa ajili ya kujadili matukio ya ukatili wa kijinsia.

Wadau waliokutanishwa na shirika hilo ni mahakimu, maafisa maendeleo ya jamii, Polisi Idara ya Upelelezi, Dawati la Jinsia, wenyeviti wa vijiji pamoja na wenyeviti wa Sauti za Wanawake ngazi za vijiji wanaopinga vitendo vya ukatili (kama ubakaji, ulawiti, ukekeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake na ukatili kwa watoto) katika vijiji 4 vya mradi na vijiji 8 vya awali vilivyopo ndani ya wilaya hiyo.

Vijiji vya sasa vya mradi ni Siuyu na Unyankhanya kutoka kata ya Siuyu, Munkinya na Damankia kutoka kata ya Dung’unyi. Kikao pia kilishirikisha wajumbe kutoka vijiji vya awali vya mradi huo, ambavyo ni na Mungaa na Unyaghumpi kutoka Kata ya Mungaa, Puma na Nkuninkana kutoka kata ya Puma, Kituntu na Utaho B kutoka kata ya Kituntu, Kipumbwiko na Dung’unyi vya kata ya Dung’unyi.  

Kikao hicho cha wadau kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilayani humo kililenga kutoa mrejesho juu ya uhitaji na utekelezaji wa haki za mwanamke na mtoto wa kike,ili kuhakikisha wanalindwa, wanatetewa na wanafurahia haki zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF nchini, Dkt.Suleiman Muttani alisema shirika hilo chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) limekuwa likitekeleza mradi wa AWARE katika kata 5 za Wilaya ya Ikungi kwa kufanya utetezi wa haki za wanawake na mtoto wa kike dhidi ya athari zitokanazo na mila na desturi kandamizi.

Alisema kwa sasa jukumu lao ni kuhakikisha wanaendeleza kasi ya utekelezaji wa mradi huo baada ya kukamilika kwa kikao cha kimkakati kilichorasimisha mradi huo kwa mwaka 2020.

Aidha, Kikao hicho kilicho wakutanisha watekelezaji wa sera na sheria kiliibua mambo mazito yahusuyo kuchelewa kwa kesi za vitendo hivyo vya ukatili na watuhumiwa kuachiwa muda mfupi baada ya kukamatwa, mambo ambayo yaliweza kujadiliwa na kutolewa majibu ya papo kwa papo kutoka kwa wahusika hasa mahakimu, polisi wa idara ya upelelezi na dawati la jinsia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo  Wilaya ya Ikungi,  George Francis na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo ya Kata ya Mungaa,  Frida Shaidi walisema kesi nyingi za matukio hayo ya ukatili wa kijinsia hasa za ubakaji zimekuwa zikikosa ushindi baada ya kukosekana kwa ushahidi.

"Kesi nyingi za ubakaji zinashindwa baada ya walalamikaji kushindwa kuja mahakamani kutoa ushahidi kufuatia walalamikaji na watuhumiwa kuelewana huko majumbani kwao" alisema Francis.

Kwa upande wao Afisa Upelelezi kutoka Kituo cha Polisi cha wilaya hiyo, Athmani Makoba na Dalahile Mahende wa Dawati la Jinsia nao kwa pamoja walisema changamoto ya walalamikaji kushindwa kwenda mahakamani kutoa ushahidi kunasababisha watuhumiwa kushinda kesi.

"Mara nyingi matukio haya hufanywa na watu wanaofahamiana ama ndugu wa karibu;pale ambapo watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani  walalamikaji hawaendi kutoa ushahidi, ambapo baada ya kulipana kienyeji ama kwa kile kinachoitwa “kumalizana” basi hakuna kinachoendelea na wakati mwingine hata tunapomuhitaji mlalamikaji aje kituoni utakuta mtuhumiwa akija na mlalamikaji tena wakiwa wamepakizana kwenye bodaboda" alisema Mahende.

 Wenyeviti wa Sauti za Wanawake ngazi za vijiji wanaoshughulikia uhamasishaji wa kupinga vitendo vya ukatili wilayani humo, walielezea kwa kina vitendo walivyoviibua na hatua walizo zichukua kwa kushirikiana na SPRF.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ikungi, Haroun Yunus Haroun alisema mfumo wa mawasiliano uliopo sasa umesaidia kwa kiwango kikubwa kuwabaini watuhumiwa na kuibua vitendo hivyo vinavyofanyika kwa siri ambapo vimepungua ukilinganisha zamani.

Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Mwedinuu Beleko alisema wakati wa changamoto ya Covid 19 kuanzia mwezi Machi hadi Julai mwaka huu, vikundi vya uhamasishaji katika jamii kwenye vijiji vya Siuyu, Unyankhanya, Munkinya, Damankia na Puma viliweza kutoa taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia 29, ambapo matukio hayo yako katika ngazi tofauti za ufuatiliaji.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post