VIGOGO, Yanga SC wamepata ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mwadui FC jioni ya leo Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Balama Elia Mapinduzi ‘Kipenseli’ aliyefunga bao hilo dakika ya sita tu ya mchezo akimalzia pasi ya Deus Kaseke baada ya shambulizi zuri lilioanzishwa na kiungo mwenzao, Haruna Niyinzoma ambalo liliokolewa na kipa wa Mwadui FC, Mahmoud Amir.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na Mbelgiji, Luc Eymael anayesaidiwa na mzawa Charles Boniface Mkwasa inafikisha pointi 54 katika mchezo wa 28, ingawa inabaki nafasi ya tatu ikizidiwa wastani wa mabao tu na Azam FC, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wanaendelea kuongoza kwa pointi zao 71 za mechi 28 pia.
Mechi nyingine ya leo, wenyeji Coastal Union wamelazimishwa sare ya 2-2 na Namungo FC jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mabao ya Coastal Union yamefungwa na Issa Abushehe dakika ya 53 na Hance Masoud dakika ya 59 wakati ya Namungo yamefungwa na George Makang’a dakika ya tatu na Abeid Athumani dakika ya 17.
Ligi Kuu itaendelea kwa mechi mbili kesho, mabingwa watetezi, Simba SC wakiwakaribisha Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa na Azam FC wakiwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
SOMA ZAIDI <<HAPA>>
Via Binzubeiry blog
SOMA ZAIDI <<HAPA>>
Via Binzubeiry blog
Social Plugin