WAZIRI WA AFYA AZINDUA MWONGOZO WA MATIBABU YA SIKOSELI

WAMJW- Dar es Salaam

Serikali imezindua mwongozo wa Taifa wa matibabu kwa watu wenye ugonjwa wa sikoseli, huku ikiagiza kuanzishwa kwa kliniki maalumu za kuchunguza ugonjwa huo katika ngazi ya wilaya na mikoa ili kuhakikisha watu wengi hasa watoto wanafikiwa.

Akizindua mwongozo huo leo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuanzishwa kwa kliniki katika ngazi za wilaya na mikoa itasaidia watu mbalimbali kupata huduma ya utambuzi ya ugonjwa wa sikoseli karibu na maeneo wanayoishi.

“Naagiza vipimo vya utambuzi kupelekwa kwenye ngazi ya wilaya na mikoa ili kila mtu aweze kuchunguzwa kama ana tatizo la sikoseli”. Amesema Waziri Ummy.

Pia, Waziri ameshauri upatikanaji salama wa damu kwa ajili ya watu wenye tatizo la ugonjwa sikoseli ili kuondoa changamoto ya tiba kwa wagonjwa mbalimbali.

Waziri wa Ummy ameshauri wananchi kufanya uchunguzi wa afya zao mapema ili kubaini kama wana ugonjwa huo kwani endapo watabaini itawasaidia kuanza matibabu mapema.

 Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya amewataka wadau wa ugonjwa huo kupunguza gharama za dawa kwani wagonjwa wengi hawezi kuzinunua.

“Naagiza pia dawa ya sikoseli ziingizwe katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili iwe rahisi kupatika kwa wagonjwa wengi”. Amesema Waziri Ummy.

Nae Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi amesema Serikali imefikia hatua kubwa ya kuanzishwa kwa mwongozo wa Taifa wa matibabu kwa wagonjwa wa sikoseli kwa kuwa utazuia vifo vingi.

Amesema vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa sikoseli, vinaweza kuzuilika endapo utagundulika mapema kwa watoto wachanga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema katika kliniki ya wagonjwa wa sikoseli, watoto 50 hadi 70 wamekuwa wakipatiwa matibabu ya ugonjwa huo wakati kwa mwezi ni wagonjwa 211 hadi 300.

“Katika kliniki ya watu wazima, kwa siku wanaonwa wagonjwa 30 hadi 40 na kwa mwezi wagonjwa 160 hadi 200 wanatibiwa hapa Muhimbili”. Amesema Prof. Museru.

Prof. Museru amesema watoto wenye ugonjwa huo wamekuwa wakipata tatizo la kupumua, damu kuganda mwilini na kiharusi.

Kauli mbiu ya mwaka huu, “Huduma Bora kwa Kila Mhitaji; Chukua hatua, panua wigo.”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post