WAZIRI KAIRUKI APONGEZA KAMPUNI YA QWIHAYA KWA UWEKEZAJI KIGOMA

Waziri Kairuki akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya Qwihaya alipofanya ziara kiwandani hapo.

Na  Francis Godwin - Mufindi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu -Uwekezaji  Angellah  Kairuki  ameeleza  kufurahishwa na kasi ya uwekezaji inayofanywa na  kampuni ya uchakataji nguzo za  umeme  ya Qwihaya General Enterprises Company Ltd  kwa  kuwekeza  viwanda  vya nguzo  katika  mikoa  mbalimbali  ukiwemo mkoa wa Kigoma na  kutaka  wadau wengine  kuelekeza  nguvu  zao  katika  mkoa wa Kigoma badala ya   kuwekeza Dar es Salaam  ,Dodoma na mikoa mingine  ambayo ni rahisi  kufikika.


 Waziri Kairuki  alitoa pongezi hizo jana baada ya kufanya ziara katika kampuni hiyo Mjini Mafinga ambapo alisema  kuwa  mkoa  wa  Kigoma  ni mkoa  ambao  upo  pembezoni na shabaha ya serikali  ni  kuendelea  kuhamasisha  na  kuwavutia  wawekezaji  wengi  zaidi kufika  kuwekeza  viwanda katika  mkoa  huo  badala ya  kuona  uwekezaji  mkubwa  ukifanyika Dar es Salaam ,Arusha ,Mwanza na mikoa mingine  ambayo  kimsingi ni  rahisi  kufikika .

Alisema kuwa  mkoa wa Kigoma  upo  pembezoni  mwa  nchini  na  wawekezaji  wengi  wamekuwa wakikwepa  kuwekeza  viwanda  vyao katika  mkoa   huo  kutokana na umbali  ila kampuni  hiyo ya Qwihaya imeweza  kufika na kuwekeza kiwanda  ndani ya  mkoa   wa Kigoma ,Njombe na Iringa jambo  ambalo ni jema na la kupongezwa  zaidi.

"Kitendo cha Qwihaya  kufika   kuwekeza  Kigoma  ni uzalendo wa hali ya  juu  na mmefungua mlango kwa   wawekezaji   wengine  kufika   kuwekeza katika  mkoa wa Kigoma maana  nako  kuna   watanzania  ambao wanahitaji kunufaika na   sekta ya uwekezaji  sio kwamba siwapongezi  kwa  kuwekeza kiwanda hapa Mafinga  mkoani  Iringa nawapongeza  pia  ila kwenda   Kigoma  mmefanya jambo zuri  zaidi  maana kupitia mkoa  wa Kigoma  mtakuwa na uwezo wa  kuuza bidhaa zenu katika  nchi  za jirani na Tanzania",alisema.

Pia  Waziri   huyo  alisema mpango  wa kampuni ya Qwihaya  wa  kufungua  kiwanda  cha kutengeneza dawa ya  kutibu  nguzo  Kibaha  ambacho kitakuwa ni  kiwanda cha kwaza  cha aina   hiyo  kwa Tanzania  kwani  alisema  kwa sasa  hakuna  kiwanda cha  dawa  ya kutibu nguzo nchini .

Akizungumzia   changamoto  za miundombinu  ya barabara ya Mgololo Mufindi  alisema kuwa  tayari TANROADS  mkoa wa  Iringa  wamekwisha  fanya  upembuzi yakinifu  juu ya barabara   hiyo na  wakati  wowote  itafanyiwa matengenezo ya  kiwango  cha lami .

Kwa  upande  wake  mkurugenzi mtendaji  wa Kampuni ya Qwihaya Leonard Maheda  alisema  kiwanda  hicho  kimeanzishwa mwaka  2007  kama   kiwanda  cha uchanaji mbao  na mwaka 2015  kilianza  kutengeneza  nguzo baada ya  kauli mbinu ya  Rais  Dkt  John Magufuli  juu ya  serikali ya  viwanda  na hata kuzuia  nguzo   kutoka nje  ya nchi .

Alisema  kiwanda  hicho  kwa mwaka  kina uwezo wa  kuzalisha nguzo 800,000 na  kuwa  nchi  nzima  wanamiliki  viwanda  vitatu  vya  nguzo  na  wanakusudia  kuanzisha  kiwanda  cha dawa  za  nguzo ambacho  kitakuwa  kiwanda  pekee  cha dawa  za  nguzo Tanzania .

Awali  akisoma  taarifa ya  kiwanda   hicho  kwa waziri Kairuki  ,Kaimu Mkurugenzi  wa kampuni ya Qwihaya General Enterprises Ltd   Benedicto Mahenda alisema  gharama  za uwekezaji  wa  kiwanda   hicho  ni takribani kiasi cha  shilingi bilioni 15.


Alisema  kwa  kipindi kirefu  kampuni  imekuwa  ikinunua malighafi  za  nguzo  kutoka  katika shamba la   miti la Sao Hill  iliyopo  chini ya TFS  na  wamekuwa  wakipata  ushirikiano mkubwa kutoka kwa   uongozi wa  shamba  hilo .

Meneja  huyo  alisema soko  la  nguzo  wamekuwa  wakitegemea  zaidi soko la ndani  kupitia  mteja mkubwa  shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na katika kipindi cha  hiki   cha utekelezaji wa  mradi wa  umeme   vijijii (REA) awamu ya tatu) soko  la nguzo  limekuwa ni kubwa  sana .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527