MATUKIO YA UDHALILISHAJI KWA WATOTO YATAJWA KUENDELEA KUTOKEA VISIWANI ZANZIBAR


Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Zanzibar Univeristy Dkt,Sikujua Omar Hamdan akiwasilisha ripoti ya matukio ya udhalilishaji kwa watoto Zanzibar kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambao uwasilishwaji huo umefanyika katika ukumbi wa watu wenye ulemavu Kikwajuni Weles Unguja.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wakifuatilia kwa umakini uwasilishwaji wa taarifa hiyo.

Muhammed Khamis-TAMWA-ZNZ
Wakati tukielekea katika siku ya maadhimisho ya Mtoto Afrika ifikapo Juni 16 mwaka huu Asasi za kiraia Visiwani Zanzibar zimesema kuna idadi kubwa ya matukio ya udhalilishaji kwa watoto visiwani Zanzibar kutoka mwaka 2017 mpaka sasa.

Akiwasilisha ripoti ya asasi hizo Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar University (ZU) Dkt,Sikujua Omar alisema kuna matukio yapatayo (1,0490) katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Akitolea ufafanuzi wa kesi hizo, alisema kesi ambazo zimetolewa hukumu kutoka mwaka 2017 hadi sasa ni (404) wakati kesi (704 ) zinaendelea na upepelezi na kesi (266) watuhumiwa hawakukutwa na hatia na kesi (59) zilikutwa na hatia.

Akitaja sababu za uwepo wa matukio hayo alisema ni pamoja na baadhi ya wanajamii kutokuwa makini na malezi ya watoto wao sambamba na kuwanunua vitu visivyokuwa muhimu na vinavyoweza kujenga ushawishi kwa watoto.

Pia alisema baadhi ya wanajamii kutokuwa na uelewa ipasavyo kuhusu matendo ya udhalilishaji na kuhisi kuwa ni vitu vya kawaida na ndiyo maana hushindwa kuwadhibiti na kuwafuatilia watoto wao majumbani.

Alieleza kuwa imekuwa kawaida kwa baadhi ya wazazi au walezi kuwafungulia milango watoto wao wa kike saa tano za usiku kwa kisingizio cha kujisomea elimu ya ziada kwa marafiki zao.

Akifafanua zaidi alisema mazingira hayo nayo pia ni sehemu hatarishi kwa watoto kufanyiwa udhalilishaji na kwamba wazazi au walezi wanapaswa kukataa mwenendo wa watoto wao.

Awali Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mohamed alisema ipo haja kubwa wakati Afrika ikielekea kuadhimisha siku hiyo jamii kubadili tabia na kutambua umuhimu wa mtoto.

Alisema kuwekwa kwa siku hiyo mahsusi ililenga kutambua umuhimu wa mtoto wa Afrika na kwamba wanapaswa kutunzwa na kuenziwa muda wote.

Alisema mtoto kama mtu mwingine anapaswa kupatiwa haki zake zote za msingi kama wanavyopatiwa wengine wote.

Meneja miradi kutoka Chama cha Waaandishi wa habari wanawake TAMWA-ZNZ Asha Abdi alisema kuna mazingira ambayo watetezi wa haki za watoto wamekua wakikutana nayo hususani kwenye kufuatilia kesi zao.

Alisema imekuwa kawaida kwa baadhi ya maafisa wa polisi kuwataka wanaofika kituoni kuwafuatilia na kuwapeleka polisi wale watu ambao wanahisi wamewatendea mabaya watoto wao.

Aidha alisema hata katika uandishi wa ripoti maalumu ya matukio hayo inayotolewa kwenye vituo vya polisi (PF3) haiweki wazi ni kitu gani mtoto anataka kupimwa anapokwenda kituo cha afya.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527