MGODI WA IRASANIRO WAUWA WACHIMBAJI WADOGO

Na Issa Mtuwa – “Wizara ya Madini” Mara

Vifo vya Wachimbaji wadogo Wawili wa madini na majeruhi Nane vilivyotokea katika kijiji cha Magunga Wilaya ya Butiama, vimemfadhahisha Waziri wa Madini Doto Biteko.  Waliofariki ni Kisambi Daudi (30) Mwikizu, mkazi wa Magunga wilaya ya Butiama na Marwa Mwita Magige (48) Mkurya mkazi wa Nyaburundu wilaya ya Bunda wamefariki usiku tarehe 11/06/2020 katika mgodi wa Irasaniro Buhemba mkoani Mara baada ya kufukiwa na kifusi na kuokolewa wakiwa wamefariki huku waliofariki wamehifadhiwa katika kituo cha Afya Nyamuswa. 

Biteko amesema chanzo vya vifo hivyo ni kutokana na ukaidi wa wachimbaji wadogo kutofuata maelekezo ya wataalamu wa madini. Amesema eneo lilitokea vifo hivyo lilizuiliwa na Mkurugenzi wa Migodi nchini Dkt. Abdruhamani Mwanga kutoka Tume ya Madini alietembelea eneo hilo siku chache zilizopita na kuzuia eneo hilo lichichimbwe kabla ya vifo hivyo kutoke.

Biteko ameongeza kuwa, pamoja na katazo hilo wachimbaji hao walikwenda usiku na kuanza kuchimba. Katika tukio hilo Mkuu wa kituo cha Polisi Buhemba Inspekta Maige alijeruhiwa kwa kupigwa na jiwe kichwani wakati akiwatawanya wachimbaji waliokuwa wamekusanyika kwenye eneo hilo kwa ajili ya usalama wao. 

 Akizungumza kwa ukali na huzuni akiwa mgodini hapo leo tarehe 12/06/2020 Biteko amesema ukaidi wa kutofuata sheria na utaratibu unaotolewa na wataalam wa madini ni ctatizo kwa wachimbaji wa madini. Ameongeza kuwa endapo wachimbaji hao wasinge kaidi maelekezo ya wataalamu madhara hayo yasingetokea.

 “Ndugu zangu mnataka nini kutoka Serikali hii, maelekezo tuliyopewa na Rais  tumetekeleza. Maeneo ya uchimbaji tumewapa, kodi lukuki tumepunguza, kero tumezitatua, mabobu ya kukimbizana kati ya Wachimbaji wadogo na wawekezaji katika utawala huu hakuna, awafanyie nini Rais John Pombe Magufuli…? 

 Wataalam wa madini walishaweka tahadhi kuhusu eneo hilo lakini wachimbaji mmekaidi na haya ndio matokeo yake” alisema Biteko  huku akihuzunishwa.

Anasema, kazi yake kubwa ni kutekeleza anachoagizwa haswa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ili fedha hizo zikatatue changamoto ya wananchi na kuleta maendeleo ya watanzania wote. Amesema Wizara yake siku zote anaongelea kuhusu Namba (takwimu) lakini sio Namba za vifo ndo maana anahuzunishwa na vifo hivyo. 

Kufuatia hali hiyo Biteko ametoa maagizo ni marufuku uchimbaji wa madini wakati wa usiku na kuiagiza ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama na kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha uchimbaji wa usiku haufanyiki na atakae kamatwa achukuliwe hatua ya kisheria.

Eneo la mgodi wa Buhemba kumekuwa na matukio ya vifo vya wachimbaji wadogo na machimbo hayo yalishawahi kufungwa kutokana na wachimbaji kufukiwa. Ufunguaji wake uliendana na utekelezaji wa masheriti waliyopewa ingawaje vifo hivyo vimetokea eneo jingine lakini hapo hapo Buhemba.  


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527