MRADI WA MAJI WA BIL 9.4 KYAKA- BUNAZI WASAINIWA


Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imesaini mkataba na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) ya China kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Kyaka- Bunazi wenye thamani ya shilingi 9,414,739,257.50.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa kusaini mkataba huo kwenye Ofisi za MWAUWASA, Jijini Mwanza, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele aliipongeza kampuni hiyo kwa kushinda tenda na alibainisha kwamba ujenzi wa mradi huo utachukua miezi 13.

Alisema mkataba unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji kwenye Mto Kagera chenye uwezo wa kuzalisha lita za maji 6,574,000 kwa siku; ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye chanzo hadi kwenye kituo cha tiba ya maji; ujenzi wa kituo cha tiba ya maji kitakachokuwa na tenki la kuhifadhia maji.

Alibainisha kwamba kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Kyaka, Bunazi na maeneo mengine yanayozunguka mradi Wilayani Missenyi.

Mhandisi Msenyele alimsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kama ilivyo kwenye mkataba. “Ni vyema Mkandarasi ukatambua suala la muda, hakikisha mradi unakamilika kwa wakati, wananchi wanausubiri huu mradi kama walivyoahidiwa,” alisisitiza Mhandisi Msenyele.

Mara baada ya kusaini mkataba, Mhandisi Msenyele alimtaka Mkandarasi kuelekea eneo la mradi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kuanza ujenzi hasa ikizingatiwa kwamba ujenzi wa mradi ulipaswa kuwa umekwisha anza.

“Hakuna sababu ya kuchelewa, mipango yote ipo tayari na kwakuwa tumekwisha saini mkataba ni vyema ukafika eneo la mradi na kujipanga ukiwa huko huko, suala la muhimu kwa sasa ni nyinyi kufika eneo la mradi,” alisisitiza Mhandisi Msenyele.

Kwa upande wake Mhandisi Mradi wa Kampuni ya CCECC, Mhandisi He Jun alimhakikishia Mhandisi Msenyele kwamba watahakikisha wanakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kama ilivyo kwenye mkataba.

Ujenzi wa mradi wa maji Kyaka Bunazi ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Julai 11, 2019.

Akiwa njiani akitokea Wilayani Karagwe kuelekea Wilayani Chato, Rais Magufuli alisimama katika Mji Mdogo wa Kyaka kusalimiana na wananchi ambao walimueleza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.

Kufuatia hali hiyo, Rais Dkt. Magufuli alimuelekeza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuhakikisha anafika eneo hilo ili kutazama namna ya kuwa na mradi utakaotumia maji kutoka Mto Kagera.

Waziri Mbarawa alifika eneo hilo na alielekeza Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) kushirikiana na Mamlaka ya Maji Bukoba na Wakala wa Maji Vijijini kuratibu upatikanaji wa mradi huo.

MWAUWASA ilipewa jukumu la kusimamia hatua zote za ujenzi wa mradi kwa niaba ya Wizara ya Maji kuanzia mchakato wa upatikanaji wa Mkandarasi atakayeutekeleza.

Aidha, Mhandisi Msenyele alibainisha kwamba japo agizo lilikuwa kuwapelekea maji wananchi wa eneo la Kyaka lakini baada ya kufanyika kwa tathmini ilionekana kuwa hata mji wa Bunazi ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Missenyi napo palikuwa na uhitaji mkubwa wa maji.

Aliongeza kuwa kufuatia tathmini hiyo, ilibidi usanifu na utayarishaji wa mradi uhusishe pia maeneo hayo mengine yaliyokuwa na uhitaji wa maji ili kujengwe mradi wenye uwezo wa kuhudumia maeneo yote na kwamba suala hilo limechangia kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa mradi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527