MAAFISA TARAFA 22 MKOANI TABORA WAKABIDHIWA PIKIPIKI ZA MAGUFULI


JUMLA ya pikipiki 22 zimekabidhiwa kwa Maafisa Tarafa 22 wa Mkoani Tabora ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa mwaka 2019 wakati alipokutana na Maafisa tarafa wote nchini katika kikao kazi jijini Dar es Salaam.

Pikipiki hizo zimekabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanri wakati wa halfa fupi ya makabidhiano.

Alimshukuru Rais kwa kutoa pikipiki hizo ambazo zitasaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Maafisa Tarafa katika maeneo yao.

Mwanri aliwataka Maafisa Tarafa walikabidhiwa pikipiki kuzitunza na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia shughuli mbalimbali Mkoani humo ili kuwasaidia Wakuu wa Wilaya kutekeleza majikumu yao kwa ufanisi.

“Hizi pikipiki ni kwa ajili ya matumizi ya Ofisi ikiwemo kwenda maeneo mbalimbali kutatua matatizo ya wanannchi na sio vinginevyo…tukikuta umetoa namba na kuigeuza Bodaboda na shughuli nyingine hazihusiani na majukumu yao ujue kuanzia siku hiyo una kazi” alisisitiza

Mwanri aliwataka Maafisa Tarafa hao kuzitumia pikipiki hizo kwa kuwafikia wananchi wote wakiwemo wakulima hasa kipindi hiki cha mavuno na lengo kuu likiwa ni kuwaasa kutunza chakula na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili.

Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu alisema wataandaa mwongozo ambao utaweka vigezo wa kusimamia pikipiki hizo ikiwemo kuhhakikisha mtumiaji amepewa mfunzo na kuwa na kitabu kinachoonyesha mzunguko na matumizi ya pikipiki hizo.

Naye Afisa Tarafa wa Ussoke Nelson Majura alimshukuru  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwawezesha kupata usafiri huo ambao utarahisisha utendaji kazi wao huku akiahidi kuwa watazitunza na kufuata maelekezo yote waliyopewa na viongozi.

Aliuomba uongozi wa Wilaya mkoani humo kuhakikisha wanasaidia mafuta na fedha matengenezo ili kusudi la kusaidiwa na Rais liweze kuzaa matunda ya kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wa Afisa Tarafa wa Tabora Kaskazini Haika Masue alimshukuru Rais kwa moyo wake wa upendo wake kwao kwa kuwapatia usafiri na vilevile kukutana nao.

Alisema watatumia pikipiki kutembelea wananchi na kusikiliza shida zao ikiwemo kutoa elimu ya kuzingatia maagizo ya wataalamu katika kujikinga na janga la Corona.

Tarafa zilizonufaika za pikipiki mkoani ni Tabora Kaskazini , Tabora kusini, Kiwele, Sikonge, Manonga, Igunga, Igurubi, Simbo, Nyasa, Bukene, na Puge.

 Nyingine ni Mwakalundi, Uyui, Igalula, Ilolangulu, Urambo, Usoke, Kaliua, Kashishi, Kazaroho, Mwongozo na Igagala.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post