NAIBU WAZIRI MABULA ATAKA WADAIWA SUGU KODI YA ARDHI KUBANWA

Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinapeleka hati za madai ya kodi ya pango la ardhi kwa wadaiwa sugu wa kodi hiyo kuanzia jumatatu tarehe 18 Mei 2020 na watakaokaidi kulipa kwa hiari wafikishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba ya Wilaya.

Dkt Mabula alitoa maagizo hayo tarehe 16 Mei 2020 akiwa katika ziara yake mkoani Iringa kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi sambamba na kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika baadhi ya Taasisi zilizopo katika halmashauri za Manispaa na wilaya ya Iringa.

Katika ziara yake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwafikia wadaiwa sugu wakubwa wa mkoa wa Iringa  ambao ni Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka mkoa wa Iringa (IRUWASA) , Shirika la Umeme mkoa wa Iringa, Benki ya CRDB, Hoteli ya Peacoc  na kituo cha Radio cha EBONY ambao kwa pamoja wanadaiwa zaidi ya milioni 128.

Dkt Mabula alizitaka idara za ardhi katika halmashauri zote nchini kupitia kumbukumbu za wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi vizuri na kuwaandikia Hati za Madai zitakazowataka wadaiwa kulipa kwa hiari madeni yao na watakaokaidi wafikishwe katika Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba ya Wilaya.

‘’ Wdaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi baada ya hati ya madai kupelekwa wawe wamelipa kodi hiyo kwa hiari ndani ya siku kumi na nne na wakishindwa wafikishwe kwenye mabaraza ya ardhi ya nyumba ya wilaya, tunataka Ikifika juni 30, 2020 Wizara iwe imekamilisha kukusanya Bilioni 180 kama ilivyojiwekea katika malengo yake’’ alisema Dkt Mabula

Akiwa ofisi za Shirika la Umene mkoa wa Iringa, Naibu Waziri wa Ardhi alimueleza Meneja wa mkoa wa Shirika hilo Richard Swai kuwa, shirika lake linadaiwa milioni 384 kama kodi ya pango la ardhi kwa kushindwa kulipa kodi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu katika eneo inalomiliki la Mtera na kutaka kupewa ahadi ya maandishi itakavyofanikisha kulipa deni hilo.

Meneja wa TANESCO Iringa Swai alieleza kuwa, eneo linalodaiwa liko chini ya idara ya Uzalishaji Makao Makuu na malipo yake hufanywa huko ambapo alimuahidi Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kulifanyia kazi suala hilo.

Kwenye ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Iringa (IRWASA) Dkt Mabula baada ya kumueleza Mkurugenzi wake Gilbert Kayange kuhusiana na deni la Mamlaka hiyo katika maeneo ya Gangilonga na Itamba linalofikia milioni 104.1, Mkurugenzi huyo alisema, Mamlaka yake  imekuwa ikilipa kodi hiyo ingawa kuna tofauti ya kiwango cha deni walichopelekewa na kumbukumbu walizo kuwa nazo jambo alilolieleza kuwa limeifanya Mamlaka yake kutaka kukaa pamoja na halmashauri husika ili  kufanya uhakiki.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Iringa kuhakikisha kufikia ijumaa tarehe 22 Mei 2020 inazipeleka Hati 110 katika Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Iringa kwa ajili ya kukamilishwa ili wamiliki wake wapatiwe hati.

Hatua hiyo inafuatia Dkt Mabula kufanya upekuzi katika Majalada ya ardhi aliyoyakuta katika ofisi ya Masijala ya Ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Iringa ambapo baadhi ya majalada hayo hayajakamilishwa toka mwaka 2019 jambo lilillomsikitisha na kuamuru majadala hayo kufanyiwa kazi haraka.

‘’Yaani hati ziko hapa tangu mwaka jana eti mnamsubiri Kamishna, huu ndiyo ucheleweshaji hati unaolalamikiwa na wananchi, nataka kufikia ijumaa ijayo majalada yote 110 yawe yamepelekwa kwa Kamishna  kwa ajili ya kuandaliwa hati’’ alisema Dkt Mabula

Aidha, aliitaka ofisi ya Msajili wa Hati mkoa wa Iringa kuhakikisha mara baada ya kukamilika uandaaji hati za ardhi, ofisi hiyo iwasiliane na halmashauri husika kwa ajili ya kuzipeleka hati hizo katika maeneo hayo kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wananchi kuzifuata mkoani.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amembana Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Hamid Njovu kurejesha kiasi cha milioni 368,100,000/= ikiwa ni sehemu ya fedha ilizokopeshwa halmashauri yake kwa ajili ya mradi wa kupanga na kupima viwanja katika manispaa hiyo.

Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilikopeshwa shilingi milioni 418,100,000 kwa jili ya mradi wa kupanga na kupima viwanja katika eneo la Igumbilo ambapo jumla ya viwanja 253 vilipimwa na kuuzwa na halmashauri hiyo ilifanikiwa kuuza viwanja 197 na kupata shilingi 692,667,000/= lakini ikarejesha kiasi cha milioni 50 pekee.

Naibu Waziri wa Ardhi alisema, mkopo uliokopeshwa halmashauri hiyo pamoja na halmashauri nyingine nchini unatakiwa kurejeshwa kwa asilimia mia moja lakini kati ya halmashauri 24 zilizokopeshwa ni halmashauri nne pekee ndizo zilizorejesha  mkopo huo kwa asilimia mioa moja na kuagiza halmashauri zilizokopeshwa kurejesha fedha hizo kama inavyoelekeza katika masharti ya mkopo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post