Picha : WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA TANZANIA ATUA MADAGASCAR KUCHUKUA DAWA YA CORONA


Tanzania imesema haijalegalega wala kujitenga katika kupambana na maradhi ya COVID – 19  na badala yake imetoa uongozi madhubuti katika kuratibu na kuunda timu ya wataalamu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kuandaa muongozo na utaratibu wa kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za kupunguza nguvu ama kuleta tiba ya COVID – 19.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo wakati akipokea msaada wa dawa inayodaiwa kutibu na kukinga ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona COVID -19 iliyotolewa na Nchi ya Madagascar kwa Tanzania.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa madai yanayotolewa kuwa Tanzania imelegalega ama kujitenga katika kupambana na ugonjwa wa COVID 19 si ya kweli kwa kuwa Tanzania imetoa uongozi madhubuti katika eneo iliyopewa dhamana ya uongozi ya Uenyekiti wa  nchi SADC na imeifanya na inaendelea kuifanya kwa heshima na bidii zote.

 Ameongeza kuwa Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa SADC tangu kuzuka kwa ugonjwa wa COVID -19 tayari imesimamia na kuratibu mikutano iliyoendeshwa kwa njia ya mtandao (Video Conferencing) kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa huo na kutoa muongozo wa jinsi ya usafirishaji wa bidhaa muhimu na kwamba mingozo hiyo imetolewa na kukubaliwa na nchi zote wanachama wa SADC

Amesema miongoni mwa masuala waliyokubaliana katika mikutano ya SADC ni pamoja na kukubaliana kuwa kila nchi ya SADC ichangie aidha katika kutafuta njia ya kusaidia kupunguza nguvu ama kuleta tiba ya COVID – 19 na Madagascar imekuwa Nchi ya kwanza miongoni mwa nchi wanachama kupiga hatua ndani ya SADC na ndani ya Afrika na kwamba katika mkutano ujao wa SADC wataitambua Madagascar kwa mchango wake wa kupambana na Virusi vya Corona.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Mhe. Tehindrazanarivelo Djacoba As Oliva amezitaka nchi za Afrika kuungana kwa pamoja kupata suluhisho la maradhi ya COVID 19 ambayo pia itakuwa suluhisho na faraja kwa dunia nzima.

Ameongeza kuwa ni faraja kwa Madagascar kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kufika nchini humo kwa ajili ya kujionea dawa hiyo jambo ambalo anaamini kukiwa na nguvu ya pamoja ndani ya SADC kuendeleza dawa hiyo na kuifanyia tafiti zaidi itakuwa mkombozi kwa Maisha ya watu wengi duniani.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi wa kulia akinywa dawa ya kutibu ugonjwa wa virusi vya corona
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Mhe. Tehindrazanarivelo Djacoba As Oliva mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Antananarivo kwa ajili ya kupokea msaada wa dawa ya kutibu na kukinga ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona uliotolewa kwa Tanzania na Nchi ya Madagascar.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527