WAZIRI WA KILIMO AWAHAKIKISHIA WATANZANIA MAVUNO YA MAZAO YATAKUWA YA KUTOSHA

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imeendelea kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula ili watu wake wawe na nguvu ya kufanya kazi kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kauli hii ya serikali imetolewa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga Tarehe 11 Aprili 2020 mkoani Songwe wakati akikagua mashamba ya wakulima mashambani.

Akiwa katika Kijiji cha Idiwili na Iyula mkoani humo Waziri Hasunga ameridhishwa na hali ya ustawi wa mazao ya wakulima shambani hivyo kuwahakikishia wananchi kuwa kutakuwa na mavuno ya kutosha katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 kwani wakulima wengi wameitikia wito wa serikali wa kuongeza tija na uzalishaji wa mazao.

Waziri Hasunga amesema kwa miaka mitatu  sasa serikali ya imeendelea kuhakikisha nchi inazalisha mazao mengi na ya kutosha ya chakula kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wizara ya kilimo na taasisi zake.

Alibainisha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula mwaka 2019 ulishuka ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo nchi ilizalisha tani milioni 16.8 hivyo katika msimu huu wa mwaka 2020 nchi itazalisha mazao ya kutosha na kuwa na utoshelevu mkubwa wa chakula

Amewapongeza wakulima nchini kwa kuitikia wito na maelekezo ya serikali katika kuhakikisha uzalishaji nchini unaendelea kuongezeka hususani kwenye mazao ya chakula na biashara.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameigiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha inaharakisha upatikanaji na usambazaji wa mbolea aina ya UREA ambayo imeadimika kwa wakulima.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amebainisha mkakati wa serikali wa kuongeza uzalishaji wa zao la Pareto ambapo umeanza mkakati wa makusudi wa kuanzisha shamba la pareto katika Kijiji cha Idiwili Mkoani Songwe kwa ajili ya uvunaji wa mbegu ili kuongeza kiasi cha mbegu kwani idadi ya wakulima inaongezeka kila siku. 

Tanzania imejaaliwa kuwa na mifumo mbalimbali ya kilimo yenye misimu ya tabia nchi inayotofautiana na hali za ekolojia ya kilimo inayofaa kwa uzalishaji wa mazao.  Mazao makuu ya chakula yanayolimwa ni pamoja na mahindi, mtama, lulu, mpunga, ngano, jamii ya kunde (hasa maharage), mihogo, mbatata, ndizi mbichi na ndizi za kuiva.  

Vyakula mbalimbali vya biashara vinavyozalishwa ni pamoja na kahawa, pamba, korosho tumbaku, katani, pareto, chai na miwa.

Mbegu za mafuta ni pamoja na karanga, alizeti na ufuta. Kilimo cha bustani hujumuisha mazao kama vile mbogamboga, matunda, maua na viungo vya chakula. Karafuu ni zao kuu la biashara kwenye visiwa vya Zanzibar.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post