Breaking : MBUNGE WA SUMVE RICHARD NDASSA AFARIKI DUNIA DODOMA...BUNGE LAAHIRISHWAMbunge wa Jimbo la Sumve mkoani Mwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Richard Ndassa maarufu Seneta amefariki dunia leo Jumatano Aprili 29,2020 mkoani Dodoma.


Spika wa Bunge, Job Ndugai, leo Aprili, 29, 2020, ameahirisha Mkutano wa 19, Kikao cha 9, cha Bunge hadi kesho, kufuatia kifo cha Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa.Ndassa anakuwa mbunge wa pili wa CCM, kufariki dunia wakati Mkutano huu wa Bunge la 19 ukiendelea, baada ya Mbunge wa Viti Maalumu Mchungaji Getrude Rwakatare kufariki dunia wiki iliyopita.

“Waheshimiwa wabunge, ninaomba kuwajulisha kuwa bunge letu limepata na msiba mwingine mkubwa wa kuondokewa na mbunge mwenzetu wa Jimbo la Sumve  ambaye amefariki usiku wa kuamkia leo hapa Dodoma.

“Kufuatia msiba huo, taratibu mbalimbali za mazishi zimeanza kufanyika kwa mawasiliano kati ya Ofisi ya Bunge na familia ya marehemu na serikali na kila tukipata taarifa zadi za kuwataarifu tutafanya hivyo,” amesema.

Aidha, akimueleze Ndassa, Spika Ndugai amesema; “Marehemu Ndassa ni mmoja wa wabunge waliokuwa wanaitwa senetors, alikuwa ni mmoja wa wabunge waandamizi walioingia bungeni tangu mwaka 1995, amekuwa mbunge wa Sumve kwa vipindi vitano na miezi… hii inaonyesha imani kubwa waliyokuwa nayo wananchi wa Sumve na wabunge wengi tunaweza tukajifunza uongozi bora kwa kufuata nyayo zake.

Pamoja na mambo mengine, Spika Ndugai amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 151 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2016, kwa siku ya leo hawataendelea na kikao cha bunge badala yake watakuwa na maombolezo ya msiba wa mbunge huyo.

“Tutajitahidi sana iwezekanavyo kuhakikisha kwamba ndugu yetu anazikwa kule Sumve kesho jioni, tutajitahidi sana sana… kwa sababu kwa mila zetu za Kiafrika kwa kweli kumzika mtu popote pale ni jambo linalotupa ugumu fikiria wote tuliopo hapa upate jambo kama hilo halafu  unawekwa popote, kwa hiyo tutajitahidi sana. Kwa hiyo ofisi yangu itashirikiana na serikali kuona kila kinachowezekana kinafanyika,” amesema Spika Ndugai.

Ndassa amekuwa Mbunge wa Sumve kwa vipindi vitano mfululizo tangu 1995. Kwahiyo (1995/2000), (2000/2005), (2005/2010), (2010/2015) na (2015/2020).

 Ni mmoja wa wabunge wa siku nyingi ambapo amekuwa bungeni miaka 25 mfululizo tangu mwaka 1995.

Ndassa aliwahi kuwa mfanyakazi wa gazeti la Mfanyakazi.


Page Liked · 30 mins 

Miaka hii mitatu imenikumbusha sana namna tulivyo viumbe dhaifu hapa duniani na kwamba hakuna jambo moja lililo la uhakika kwenye maisha yetu. Maana leo upo, na kesho haupo. Sekunde hii Mzima, na ijayo hujui nini kitatokea. Tuswali sana na kuomba radhi za Allah ndugu zangu. RIP Mzee wangu, Mhe. Ndasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post