LHRC YAZINDUA RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA 2019



Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga (katikati), Afisa Utafiti, Fundikila Wazambi (kushoto) na Mkurugenzi wa Uwajibikaji na Uwezeshaji wa Kituo hicho, Felista Mauya (kulia) wakionesha nakala za Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2019 mara baada ya uzinduzi leo Aprili 29, 2020 katika ofisi za LHRC jijini Dar es Salaam na wadau kufuatilia kwa njia ya mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga (katikati) akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2019. Uzinduzi huo uliofanyika  leo Aprili 29, 2020 katika ofisi za LHRC jijini Dar es Salaam na wadau kufuatilia kwa njia ya mtandao.

***
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezindua Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2019 inayoangazia hali ya haki za binadamu kwa mwaka 2019 na kufanya ulinganisho wa hali ilivyokuwa mwaka 2018. 

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano, Aprili 29, 2020 kwa njia ya mtandao kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC amesema ripoti hiyo inahusisha matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu sambamba na mapendekezo kwa ajili ya uboreshaji wa sera, sheria na utendaji katika jamii. 

Anna amesema ripoti hiyo inaangazia hali ya haki za binadamu katika nyanja za haki za kiraia na kisiasa; haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni; haki za makundi yaliyo hatarini; mifumo ya Ulinzi wa Haki za binadamu na haki za kijumla.

“Ripoti hii ni matokeo ya taarifa mbalimbali zilizokusanywa na LHRC ikiwemo taarifa kutoka kwa waangalizi wa haki za binadamu walio nchi nzima, wasaidizi wa kisheria walio katika wilaya mbalimbali, taarifa rasmi toka taasisi za Serikali, Bunge, Mahakama, jeshi la polisi, vyombo vya habari na asasi mbalimbali za kiraia zisizo za Serikali. Taarifa hii pia hutumia taarifa mbalimbali za kitaifa lakini pia na za kimataifa, hasa zinazolenga kuelezea hali ya haki za binadamu nchini”, amesema Anna Henga.

Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2019 ni muendelezo wa ripoti za kituo hicho zinazotolewa kila mwaka kwa lengo la kuonesha hali na kutoa mapendekezo ya maboresho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527