UJENZI WA SGR WAENDELEA KWA KASI, TRILIONI 2.957ZATUMIKA HADI SASA


Na Frank Mvungi- MAELEZO
Serikali imetumia kiasi cha Shilingi Trilioni 2.957 kutekeleza mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) huku kasi ya utekelezaji ikiongezeka.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma , Msemaji Mkuu wa Serikali  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendelea kama ulivyopangwa.

“Mradi  wa SGR kwa kipande cha Dar es Salaam na Morogoro umefikia asilimia asilimia 75 wakati kipande cha Morogoro Makutopora Singida kimefikia takribani asilimia 28”, Alisisitiza Dkt. Abbasi

Akifafanua Dkt. Abbasi amesema kuwa watanzania wataanza kutumia usafiri huo wa kisasa kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro mwaka huu wa 2020 hivyo ile ahadi ya Serikali kwa wananchi itatimia kama ilivyopangwa na kwa wakati.

Kwa upande wa kipande cha Mwanza-Isaka  Dkt.Abbasi amesema kuwa wakati wowote tenda itatangazwa ili kumpata mkandarasi atakayejenga reli hiyo kwa kipande hicho ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.  Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa mwezi Desemba 2019 Jijini Mwanza kwa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.

Akizungumzia baadhi ya wanasiasa wanaobeza juhudi za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi kama SGR Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali haitarudi nyuma katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwa hata wanaobeza watanufaika na miradi hiyo ikiwemo ndege na umeme.

Kwa upande wa utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere(JNHPP) , ujenzi wa eneo la kuchepusha maji ya mto Rufiji ili ujenzi wa ukuta wa bwawa uanze limekamilika kwa asilimia mia moja,  Aidha bwawa hilo linatajwa kuwa kati ya mabwawa makubwa 70 ya kuzalisha umeme wa maji Duniani na kwa Afrika litakuwa la nne kwa ukubwa.

Kwa upande wa kiwango cha fedha kilicholipwa hadi hasa Dkt. Abbasi amesema kuwa Shilingi Trilioni 1.275 kati ya Trilioni 6.5 zimeshalipwa ambapo kazi zote zinaendelea kama ilivyopangwa.

Katika hatua nyingine Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara zote kesho Machi 2, 2020 na watatembelea mradi wa SGR  ili kujionea utekelezaji wake.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa Chelezo katika Ziwa Victoria Dkt. Abbasi  amesema kuwa umekamilika kwa asilimia 100 na Shilingi Bilioni 32.8 zimeshalipwa na katikati ya mwezi Machi Itaanza kufanya kazi , huku ukarabati wa MV Victoria umefikia asilimia 89 na Bilioni 14 zimeshalipwa, Wakati MV Butiama ukarabati wake umefikia asilimia 86 na Bilioni 3 zimeshalipwa kati ya Bilioni 4 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo.

“ Ujenzi wa meli mpya  na ya kisasa katika Ziwa Victoria itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na Tani 400 za mizigo umefikia asilimia 52 hadi sasa na unaendelea kutekelezwa kwa kasi kama ilivyopangwa.

Utaratibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali kukutana na vyombo vya habari unalenga kuileta Serikali kwa pamoja na wananchi kwa kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa maslahi yao katika maeneo mbalimbali hapa nchini


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527