TAMAA YA FEDHA YAMPONZA AFISA MADINI,ASWEKWA RUMANDE

Na John Walter-Manyara

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Manyara inamshikilia Afisa Madini mkoa wa Kimadini Simanjiro,Dauda Ntalima kwa tuhuma za Kuomba Rushwa ya Shilingi Milioni tano kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One.

Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi Machi 5, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Holle Makungu alisema kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11 ya mwaka 2007.

Makungu amesema Uchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara umebaini kuwa Kampuni ya Tanzanite One inayofanya shughuli zake eneo la Mererani wilayani Simanjiro kwa sasa imesitishiwa shughuli za uchimbaji kutokana na majadiliano yanayoendelea kati yake na serikali ya Tanzania kuhusu mikataba ya uchimbaji hivyo Ntalima ambaye majukumu yake ni pamoja na kushughulikia leseni za biashara ya madini na shughuli zote za uchimbaji wa madini wilayani humo, akatumia mwanya huo kuomba rushwa hiyo kutoka kwa mkurugenzi wa Tanzanite One akidai kwamba hatima ya Mikataba ya kampuni hiyo ipo mikononi mwake.

Aidha Mkungu alisema baada ya Mkurugenzi wa Tanzanite One ambaye hakumtaja majina kwa sababu za kiuchunguzi kugoma kutoa rushwa hiyo, Ntalima aliandaa tangazo akipiga marufuku wakurugenzi wote wa Tanzanite One na viongozi waandamizi sita wa kampuni hiyo kuingia na kufanya shughuli yeyote ndani ya ukuta wa machimbo ya Tanzanite Mererani bila kibali chake.

Ameeleza kuwa mbinu waliyoitumia kumbaini mtuhumiwa huyo ni za  kiintelinsia.

Makungu amesema, Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara uchunguzi  utakapokamilika kujibu tuhuma zinazomkabili.

Ametoa wito kwa wakazi wa Manyara na watanzania wote kuendelea kufichua vitendo vya Rushwa kwa kutoa taarifa katika ofisi za TAKUKURU zilizoko kila wilaya au kupiga namba ya dharura 113.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post