MBOWE ATHIBITISHA MWANAE KUPATA VIRUSI VYA CORONA


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amethibitisha mtoto wake Dudley amepata maambukizi ya Corona.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mbowe,  Jumanne Machi 24, Dudley amethibitika kuwa na virusi vya corona baada ya kupata homa za vipindi, kuumwa kichwa mfululizo na kukohoa kwa siku tano.

“Mama yake ambaye ni daktari alibaini hali hiyo na alizitaarifu mamlaka za Serikali zinazoshughulikia janga hili nazo zilimtaka kijana apelekwe Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam kwenye vipimo zaidi ambapo ilithibitika rasmi kuwa ana virusi vya corona.

“Aidha, timu ya Serikali imeendelea kutoa ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu kwa familia yote ikiwamo ushauri nasaha kwa wanafamilia na marafiki wengine waliokutana na Dudley katika mikusanyiko mbalimbali ikiwamo kuweka wengine karantini,” amesema Mbowe.

Aidha, amesema familia yake inakiri kupokea ushirikiano wa kiwango kilichowezekana kutoka kwa mamlaka husika za Serikali wakiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu wake, Mganga Mkuu wa Serikali na wataalam wao wote.

‘Hali ya Dudley sasa imeimarika. Homa zimekwisha. Kichwa kimepona. Bado anakohoa kiasi na yuko chini ya uangalizi maalum.

‘Dudley hajasafiri nje ya nchi mwaka huu. Maambukizi haya kayapata ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Ugonjwa huu haupaswi kuwa siri japo kuna miiko inayoongoza utoaji wa taarifa za wagonjwa. Tatizo ni kubwa kuliko tulivyojiandaa na tunavyojiandaa.

‘Wengi wameitafuta familia kutaka kujua ukweli na undani wa jambo hili. Pengine kupitia ushuhuda wangu, tutaweza kuokoa wengi katika nchi yetu. Hakika leo kila mmoja anastahili kujua janga hili liko mlangoni mwake,” alieleza Mbowe kwenye taarifa yake.

Pamoja na mambo mengine, ametoa rai kwa Rais John Magufuli, kuunda timu ya kumsaidia na ashirikishe wadau wengine nje ya Serikali  kwani yako mengi ya kufanya nje ya mikakati ya kitabibu inayosimamiwa na Waziri Mkuu na Waziri Ummy Mwalimu.

“Tusiiachie serikali pekee. Tutajuta. Tusiilaumu tu, tuishauri nayo iwe tayari kuupokea ushauri na ishirikishe. Ni janga la dunia na hakika tutaumizwa kuliko tunavyowaza.

“Katika maisha maandalizi hayajawahi kuwa hasara, bali hasara iliyo majuto ni kutokujiandaa na kupuuza yanayofanywa na walioyapitia kama ilivyo nchi za wenzetu zilizoendelea na hata majirani zetu" Alisema


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527