MWAMPOSA ATANGAZA KUSITISHA MAKONGAMANO YAKE KUTOKANA NA TUKIO LA WATU 20 KUFARIKI KWA KUKANYAGANA


Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Nabii na Mtume Boniface Mwamposa amesema kwa sasa amesitisha makongamano yote kutokana na tukio lililotokea hivi karibuni lililosababisha vifo vya watu 20.
 

Mwamposa  amesema hayo leo Jumapili Februari 09, 2020 katika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe muda mfupi kabla ya kuanza ibada  ya Jumapili ambayo amesema ni ya upako, ya kufunguliwa na kuponywa.

Watu 20 walifariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa Jumamosi Februari Mosi, 2020 mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro waliposhiriki ibada ya kiongozi huyo katika uwanja wa Majengo, wakigombea kukanyaga mafuta ya upako yaliyomwagwa milango ya kutokea uwanjani.



“Makongamano mengi nimeyasimamisha kwanza. Tunaomba neema ya Mungu ikapate kusimama na watu, na baada hapo ndipo nitaweka ratiba ya makongamano. Leo lilikuwa liwe kongamano kubwa la kukanyaga mafuta, kwa sababu ya shida iliyotokea tulisimamisha yote, tunataka utulivu na kumuomba Mungu atupe neema ya kupanga mipango mipya.” amesema Nabii na Mtume Mwamposa.

Ametoa pole kwa Watanzania wote kufuatia tukio hilo la Waumini kukanyagana na hatimaye kusababisha vifo na kuongeza kuwa anatambua kuwa tukio hilo limewaumiza Watu wengi pamoja na Serikali.

“Namuachia Mungu yeye mwenyewe asimame, kwa sababu lilikuwa jambo sio dogo, ni zito, limewaumiza Watanzania, serikali imeumia, viongozi wameumia lakini mengi tutayajua hapo mbeleni,” ameeleza Kiongozi huyo wa Kanisa la Inuka Uangaze.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post