WAKUU WA SHULE WATAKIWA KUSIMAMIA TAALUMA BADALA YA KUSHINDA KWENYE OFISI ZA HALMASHAURI

Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari Mkoani Shinyanga wametakiwa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule zao badala ya muda mwingi kuutumia kwenye Ofisi za Halmashauri.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack mapema leo tarehe 04 Februari, 2020 kwenye kikao cha pamoja na Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari, Maafisa Elimu kata na Watendaji wa kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, kilichofanyika katika shule ya sekondari Mwalimu Nyerere ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa shughuli za elimu Wilaya ya Kahama,.

Mhe. Telack ambaye amefanya ziara katika baadhi ya shule hapo jana tarehe 03/02/2020 kabla la kikao hicho amebaini changamoto mbalimbali ikiwemo Wakuu wa shule kutofuatilia hali ya ufundishaji shuleni kuanzia kwa walimu hadi wanafunzi hali iliyochangia kushuka kwa ufaulu.

“Rudini mkasimamie ufundishaji na ujifunzaji, nataka tutoke hapa tulipo. Wakuu wa shule badilikeni, fungueni milango ofisi zenu ziwe rafiki kwa walimu, wazazi na wanafunzi. Maafisa Elimu hakuna kuita Wakuu wa shule Halmashauri waacheni wasimamie taaluma kwenye shule zao ” amesisitiza Telack.

Aidha, amewataka Wakuu wa shule kujiepusha na urafiki katika kazi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima badala yake wahakikishe kunakuwa na mahusiano mazuri ya kikazi.

Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya elimu, ambaye ni Afisa elimu Mkoa Bw. Mohamed Kahundi amewataka Wakuu wa shule kuhakikisha wanakuwa na miongozo yote inayohitajika ili kuwasaidia kufuatilia ufundishaji.

Nao baadhi ya Walimu wakuu na Maafisa elimu kata wamemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuyafanyia kazi yale yote aliyowaelekeza na kumuomba kuwasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili ikiwemo uhaba wa walimu, miundombinu na kutopandishwa madaraja kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza na Walimu Wakuu, Maafisa elimu wa kata na Watendaji wa kata (Hawapo pichani) wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala leo tarehe 04/ 02/2020 katika ukumbi wa shule ya sekondari Mwalimu Nyerere
Baadhi ya washiriki wa kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Watendaji wa kata, Maafisa Elimu kata na Walimu Wakuu wa shule za msingi na sekondari wakimsikiliza kwa makini (hayupo pichani) leo katika ukumbi wa shule ya sekondari Mwalimu Nyerere
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha (kushoto), katika shule ya sekondari Isaka, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Wilaya ya Kahama wakikagua nyaraka za maandalio ya masomo kwenye ofisi ya walimu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akimuhoji mtoto James Jeremia aliyedai hawezi kusoma licha kufaulu mtihani wa darasa la saba na kupelekwa shuleni na baba yake Bw. Jeremia James hapo jana tarehe 03/02/2020 katika shule ya sekondari Mwakata. Mhe. Telack ameagiza mtoto huyo aanze masomo shuleni hapo mara moja
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha akitoa neno kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack (kulia) kuzungumza na walimu Wakuu, Maafisa Elimu kata na Watendaji wa kata Halmashauri ya Wilaya ya Msalala
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bw. Mohamed Kahundi, akizungumza katika kikao hicho leo tarehe 04/02/2020
Mwalimu Dotto Mayiga wa shule ya msingi Kakola B, akizungumza katika kikao hicho

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post