WAZIRI MABULA AITAKA BODI YA NHC KUPITIA UPYA GHARAMA ZA NYUMBA INAZOUZA

Na Munir Shemweta, WANMM MASASI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kupitia upya gharama za nyumba zake ilizojenga maeneo ya pembezoni kwa ajili ya kuziuza.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana wilayani Masasi mkoa wa Mtwara wakati alipotembelea mradi wa nyumba 54 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mikoa ya Kusini pamoja na kutembelea miradi inayofanywa na NHC katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inafuatia kulalamikiwa na wabunge wa Majimbo ya Masasi Dkt Rashid Chuachua na yule wa jimbo la Lulindi  mkoani Mtwara Jerome Bwanausi kuwa pamoja na halmashauri kuhitaji nyumba kwa ajili ya watumishi lakini gharama imekuwa kubwa kiasi cha halmashauri na wananchi kushindwa kuzinunua.

‘’ Ni vizuri bodi ikae iangalia namna ya kupitia upya gharama za nyumba zote zilizopo maeneo ya pembezoni kama hizi za Masasi maana zikiachwe bila kununuliwa itakuwa ni hasara’’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri Mabula alisema, hata kama nyumba hizo zilizojengwa kwa ajili ya kuuza hazitanunuliwa basi NHC iangaliae namna ya kuzipangisha na kueleza uhitaji wa nyumba katika eneo la Masasi upo na watumisi wa serikali wanahitaji kuisha maeneo rafiki.

Hata hivyo, amezitaka halmashauri nchini kulitumia Shirika la Nyumba la Taifa kujenga miradi ya nyumba za watumishi kulingana na mahitaji ili kuepuka kujenga nyumba ambazo mwisho wa siku zinaweza zisinunuliwe.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa Muungano Saguya alisema shirika lake liko katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo uliokuwa umesimama kwa muda ambapo takriban milioni 600 zitatumika kuukamilisha na kusisitiza imani yake katika kipindi cha miezi sita ujenzi utakamilika.

Kwa mujibu wa Saguya, bei inayolalamikiwa ya shilingi milioni 54 kwa nyumba moja inatokana na gharama kubwa iliyotumiwa na Shirika la Nyumba la Taifa kuzijenga nyumba hizo na kubainisha kuwa NHC iko mbioni kuzipangisha baadhi ya nyumba ambazo wananchi wameonesha nia ya kupanga.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alizitembea wilaya za Nanyumbu na Tunduru na kukagua utendaji kazi katika sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya hizo.

Dkt Mabula alibaini utunzaji mbovu wa kumbukumbu za majala ya ardhi pamoja na kiasi kidogo cha makusanyo ya maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi ambapo aliziagiza halmashauri za Nanyumbu na Tunduru kuongeza kasi ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi sambamba na kuzingatia utunzaji majalada ya ardhi kwa kufuata taratibu ikiwemo kuwepo mawasiliano katika majalada hayo kutoka afisa mmoja kwenda kwa mwingine.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post