TANZANIA KUANZA KUTUMIA VIWANGO VYA KIMATAIFA VYA USIMAMIZI WA MALI

Na Farida Ramadhani, Dodoma
Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kuanza rasmi kurasimisha Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali (ISO 55000 Series) ili kuongeza ufanisi na ubora katika usimamizi wa mali za Umma.


Hayo yameelezwa na Kaimu Kamishna wa Bajeti, Bw.  Balandya Elikana kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, katika uzinduzi wa kikao cha kukusanya maoni ya wadau kuhusu taarifa ya tathmini ya utayari wa Sekta ya Umma Tanzania kutumia mfumo wa  Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali (ISO 55000 Series).

Bw. Elikana alisema kuwa Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali vinalenga kutoa muongozo katika sekta ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa kuainisha mahitaji muhimu ya usimamizi wa mali za Umma pamoja na namna bora ya usimamizi wa mali hizo.

“Utumiaji wa Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali ni muhimu kwa Tanzania hususan katika kipindi hiki ambacho nchi ipo katika harakati za kuwa na uchumi wa kati”alisema Bw. Elikana

Alibainisha kuwa kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wadau pamoja na Washirika wa Maendeleo kupitia Mradi wa Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) imefanya tathmini na kuandaa mpango wa utumiaji wa viwango vya kimataifa katika usimamizi wa mali.

“Leo ni sehemu ya kukamilisha kazi kwa kukusanya maoni ya wadau na kuyachambua ili kuweza kuboresha rasimu ya taarifa ya tathmini iliyofanyika pamoja na mpango kazi ambao Tanzania itaufuata katika kutumia Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali”, alifafanua Bw. Elikana.

Alisema kuwa Tanzania itapata faida mbalimbali kwa kufuata viwango vya kimataifa vya usimamizi wa mali ikiwemo, kuimarisha usimamizi wa Mali na kufanya ulinganifu wa Usimamizi wa Mali kwa Viwango vya Kimataifa pamoja na kurahisisha uwekaji wa vipaumbele kwenye usimamizi wa mali husika.

Bw. Elikana alisema faida nyingine ni kupunguza gharama ya matengenezo ya mali, kuboresha utoaji huduma, kurahisisha utoaji wa maamuzi, kurahisisha ukaguzi wa vihatarishi pamoja na kuendana na mahitaji ya viwango vingine vya kimataifa.

“Usimamizi wa mali za umma ni wajibu wa kila mwananchi na linapaswa  kutekelezwa kwa uadilifu na kwa weledi mkubwa, na ninatoa wito kwa washiriki wote katika kikao hiki kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha tathmini na mpango kazi ulioandaliwa”alisisitiza Bw. Elikana.

Naye Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Chotto Sendo alisema kuwa usimamizi wa mali za Serikali ni jukumu la muhimu kwa maendeleo ya nchi na Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali vitaongeza ufanisi.

“Usimamizi wa mali za Serikali umeanza muda mrefu lakini suala la utumiaji wa mifumo ya usimamizi huo bado haijaanza kutumika kikamilifu, kuanza kutumika kwa Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali kutaleta ahueni”, alifafanua.

Kwa upande wake Kamishana wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Frederick Mwakibinga, alisema kuwa uwekezaji wa Serikali ni mkubwa na anaamini maoni ya kikao hicho yatasaidia kutatua baadhi ya changamoto za usimamizi wa mali hizo.

Viwango vya Kimataifa vya Usimamizi wa Mali vilitangazwa rasmi kuwa sehemu ya viwango vya kimataifa na Shirikisho la Viwango vya Kimataifa (International Organisation for Standardisation) mwaka 2014 baada ya kuridhishwa na nchi wanachama 32, na kwa sasa viwango hivyo vinatumika kwenye nchi zaidi ya 41 ikiwemo Botswana, Japan, India, Canada na Uingereza.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527