RAIS MAGUFULI ARUHUSU MAKONTENA YENYE MCHANGA WA MADINI YARUDI KATIKA KAMPUNI YA TWIGA ILI YAUZWE


Rais Magufuli ameruhusu makontena yenye mchanga wa madini ya dhahabu kuuzwa, akibainisha kuwa tayari mteja amepatikana na ameshatoa kiasi kidogo cha fedha.Mwaka 2017 Serikali ya Tanzania iliyashikilia na kuzuia makontena hayo ya mchanga kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata mabaki ya madini yaliyoshindikana baada ya hatua ya kwanza ya uchenjuaji kufanyika mgodini.

Akizungumza leo Ijumaa Januari 24, 2020 katika hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kamati ya madini ya Barrick yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam Rais Magufuli amesema uuzwaji huo utakuwa na faida kwa sababu ya makubaliano hayo.“Hata yale makontena tuliyoyashika sasa fanyeni utaratibu mzuri yarudi katika Kampuni ya Twiga mtafute wateja. Najua yameshauzwa na mteja yupo na ameshalipa kiasi fulani. Pamoja na stori kuwa zilikuwa zinapelekwa kuyeyushwa. Si kweli, yalikuwa yanauzwa."

Huku akiihakikishia ulinzi kampuni ya Barrick Gold, Rais Magufuli amesema hakuweza kuvumilia kuwa rais huku rasilimali za Watanzania zikisombwa.

“Dhahabu iliwekwa Tanzania na siyo sehemu nyingine, aliyeiweka ana makusudi yake. Kwa hiyo ikisombwa bila Watanzania kupata faida ya hicho kinachosombwa, hicho ndio kinaumiza .


“Siwezi kuwa rais na mali inasombwa mnaambiwa ni mchanga, mnakubali na polisi wanasindikiza. Sasa kama ni mchanga kwanini unalindwa? Na kuzunguka eneo la mgodi watu wana njaa, hawana elimu, madawa wala maji. Haikuwa sawa,” alisema na kuongeza;


“Sisi hatupo hapa kugombana na mwekezaji yeyote, tupo hapa kushirikiana nao katika hali ya kila upande kushinda. Barrick muwe na uhakika hapa ni mahali pa kukaa, mtakaa hapa leo, kesho na daima kwa sababu tunaona nyie ni wadau wazuri.

“Nawashukuru Barrick kwa busara, mngeweza kusema tunatumia ‘force’ ila sina hakika kama mngeichimba hiyo dhahabu. Sina hakika, lakini mmetumia busara, hiyo ni nzuri sana na serikali yangu itoa ushirikiano mzuri sana ili mchimbe mpate faida na sisi tufaidike.  Fikiria kutoka ‘share’ ya sifuri hadi ya 16%, lakini pia faida itakayopatikana ni 50 kwa 50 ni ushindi mkubwa kwa pande zote mbili."


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post