PROF. KABUDI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI WA UNICEF


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.


Waziri Kabudi amemweleza Bi. Shalini Bahuguna kuwa UNICEF imekuwa na mchango mkubwa sana kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukuza, kulinda na kutimiza haki za watoto.

“Kwa ujumla UNICEF imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za maendeleo endelevu ya kulinda, kukuza na kutunza haki za watoto…..na tunaamini watoto hawa ni taifa la kesho”. Amesema Prof. Kabudi.

Waziri Kabudi amemueleza Bi. Bahuguna kuwa tangu mwaka 2016 Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNICEF, imefanikiwa kuboresha sekta za elimu na afya ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma bora za kijamii, kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na kuboresha huduma za maji katika mikoa mbalimbali ikiwemo, Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Kigoma, Njombe na Songwe.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini, Bi. Bahuguna amesema kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea
kulinda haki za watoto.

“Haki za watoto katika taifa ni jambo muhimu sana, hivyo UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu”. Amesema Bi. Bahuguna.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527