Maafisa Tarafa Nchini Watakiwa Kushiriki Vikao Vya Kamati Za Kudumu Na Baraza La Madiwani Ili Kusimamia Vyema Shughuli Za Maendeleo

Na Happiness Shayo, Iramba-Singida
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka Maafisa Tarafa nchini kushiriki vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la Madiwani ili kurahisisha utendaji kazi hasa katika usimamizi wa  shughuli za maendeleo katika maeneo yao ya kazi.

Agizo hilo amelitoa wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya kutembelea  wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.

“Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uwajibikaji wa Makatibu Tarafa katika Wilaya na Halmashauri za Serikali za Mitaa wa mwaka 2003 ni haki ya msingi kwa Afisa Tarafa kuhudhuria vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la Madiwani vya Halmashauri ili kutoa ushauri  pamoja na taarifa za utekelezaji wa shughuli zilizofanyika katika eneo lake” Dkt. Mwanjelwa amefafanua.

Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa Maafisa Tarafa wasipopewa nafasi za kushiriki katika vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la Madiwani, hoja za msingi za kimaendeleo hazitawasilishwa hivyo maendeleo yatakwamishwa katika halmashauri wanazozihudumia.

Dkt. Mwanjelwa ameweka bayana kuwa ni muhimu Maafisa Tarafa, Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Halmashauri wakafanya kazi kwa kushirikiana ili kuongeza ufanisi katika shughuli za maendeleo.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka Watendaji wa Halmashauri kujenga utaratibu wa kufanya vikao na watumishi ili kusikiliza kero zao na kuzitatua.

“Hakikisheni mnatenga muda wa kuongea na Watumishi walio chini yenu ili kuwaelimisha kuhusu nyaraka mbalimbali za kiutumishi pamoja na kusikiliza kero na maoni yao na kuyafanyia kazi” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Mhe.Dkt. Mwanjelwa yupo katika ziara ya kikazi Mkoani Singida kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments