Iran Yagoma Kuipa Marekani "Black Box" Ya Ndege ya Ukraine Iliyoanguka Jana

Iran imesema kuwa haitakabidhi kisanduku cha kunakili safari ya ndege ama ''Black box'' ya ndege ya Ukraine iliyopata ajali na kuua watu 176, kwa kiwanda kilichotengeneza ndege hiyo au kwa Marekani.

Ndege hiyo ya Ukraine aina ya Boeing 737-800 ilianguka muda mfupi baada ya kuanza safari yake kutokea uwanja wa ndege wa Tehran, na hakuna mtu aliyenusurika katika ajali hiyo.

Kwa mujibu wa sheria za anga za kimataifa , Iran ina haki ya kufanya uchunguzi kuhusu ajali hiyo.

Lakini watengenezaji wa ndege hiyo kwa ushirikiano na wataalamu kutoka nchi kadhaa wanaweza kuchunguza kisanduku hicho.

Ajali hiyo imetokea wakati ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya Marekani na Iran, muda mfupi baada ya Iran kushambulia kwa makombora kambi mbili za kijeshi za Marekani zilizopo Iraq.

Aidha hakuna ushahidi kuwa matukio haya mawili yanahusiana na kuanguka kwa ndege hiyo.

Kwa kawaida, bodi ya Marekani ya usafirishaji salama ina jukumu la kuchunguza masuala yeyote ya kimataifa yanayohusisha ndege aina ya Boeing iliyotengenezwa Marekani kwa idhini ya sheria za nchi husika.

Kiongozi wa shirika la anga Iran Ali Abedzadeh alinukuliwa katika vyombo vya habari nchini humo akisema:"Hatutawapa kisanduku cheusi kampuni iliyotengeneza ndege hiyo au Wamarekani"

"Tukio hilo litachunguzwa na shirika la anga la Iran lakini Ukraine itaruhusiwa kuwepo katika uchunguzi huo" 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments