KATIBU MKUU CCM: UCHAGUZI SIO NAMBA, NI MAAMUZI YA UMMA


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amewakumbusha baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini maana halisi ya uchaguzi ni maamuzi ya Umma si kama ambavyo wamekuwa wakieleza kwa kupotosha kuwa, uchaguzi ni namba.


Ameyasema hayo tarehe 13 Januari, 2020 alipokuwa akihutubia viongozi wa mashina,matawi, Kata na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya wilaya za Handeni na Kilindi Mkoani Tanga.

“Nimewasikia baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wanasema uchaguzi ni namba. Uchaguzi sio namba, uchaguzi ni uamuzi wa umma, namba ni kitu cha baadae, waambieni wanaosema uchaguzi ni namba waache kugeuza uchaguzi kama mchezo wa kamari au bingo, uchaguzi ni uamuzi wa wananchi juu ya mustakabali wao.”

Amesisitiza zaidi kuwa, wananchi hufanya hivyo kabla ya siku ya kupiga kura, siku ya kupiga kura ndio siku ya kudhihirisha uamuzi wao, lakini uamuzi wao huanza kufanyika tangu uchaguzi ulipoisha.

Hivyo Katibu Mkuu ameeeleza kuwa, CCM inauona uchaguzi kama zoezi muhimu sana linalohusu uamuzi wa wananchi juu ya mustakabali wa taifa lao, uamuzi wa wananchi juu ya wananchi wenzao wanaofaa kuwaongoza kwa maendeleo yao, uamuzi wa wananchi juu ya chama chenye sifa, kinachoaminika, kinachoweza, chenye rekodi ya kuongoza nchi na sio vinginevyo.

Wakati huo huo Dkt. Bashiru amewahakikishia wananchi msimamo wa CCM kuendelea kuisimamia serikali kutekeleza kila kilichoahidiwa na kisichotekelezwa huelezwa ni kwa nini hakijatekelezwa, hivyo mwaka huu ni mwaka wa wanaCCM wote kuueleza umma yote yalioahidiwa yametekelezwa kwa kiasi gani, yepi yametekelezwa vizuri, yepi yametekelezwa kwa wastani na yepi ambayo Chama kitaongeza nguvu zaidi.

Aidha Katibu Mkuu ametumia mkutano huo wa ndani kuwataka wenyeviti wa Vijiji na Mitaa, watendaji wa mitaa na Halmashauri, kuwa wabunifu na kung’amua fursa za maendeleo, na kwa wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia ubunifu kwa watendaji ili kuwawezesha wananchi kupiga hatua kwa haraka.

Viongozi mbalimbali wakizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, wameonesha kuridhishwa na kasi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM licha ya changamoto mbalimbali ambazo wanaendelea kuzishughulikia na kuzitafutia majawabu ikiwa ni pamoja na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini.

Mkutano huo umehudhuriwa na wanachama, viongozi wa Chama na Serikali wakiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ndg. Mohamed Salim Ratco (MNEC), Mkuu wa Mkoa wa Tanga Ndg. Martin Shigela, wajumbe wengine wa Halmashauri Kuu Bi. Mwantumu Zodo, na Bi. Catherine Kitandura na wabunge wa Mkoa wa Tanga.

Katibu Mkuu yupo Mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku nne, ambapo ziara hiyo imelenga kuimarisha na kuhuisha uhai wa Chama katika ngazi za Mashina na Matawi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post