SERIKALI KUZALISHA ZAIDI YA TANI ELFU HAMSINI TATU ZA MBEGU MWAKA 2019/2020

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Serikali nimewema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/20 kwa kushirikiana na sekta binafsi, imejipanga kuzalisha jumla ya tani 53,608.2 za mbegu mbalimbali.

Wazalishaji hao ni pamoja na Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA), Vituo vya Utafiti, Magereza na Sekta binafsi. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea na ujenzi wa Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 2 Novemba 2019 wakati akifunga mradi wa ubia kwa maendeleo ya mifumo ya uzalishaji endelevu wa mpunga Afrika chini ya jangwa la Sahara wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Amesema kuwa Sanjali na jitihada hizo, Wizara ya Kilimo imeanzisha kitengo cha masoko ya mazao ya kilimo ambacho kinahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa mazao mbali mbali yanayozalishwa hapa nchini ili mbegu zitakazozalishwa na kuwa na mafanikio makubwa katika kilimo uweze kuimarisha kipato cha wananchi.

Takwimu zinaonesha kwamba wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya  matrekta na asilimia 24 ya wanyama kazi mwaka 2013.

Amesema kuwa Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua na kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa mwaka 2013.  Aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara imeendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo.

Mhe Hasunga amesema kuwa pamoja na hayo, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika kwa kusimamia na kuhamasisha maendeleo yake hapa nchini ili wakulima waweze kunufaika na matunda ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika usimamizi madhubuti wa sekta ya ushirika.

Ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo imeendelea kuratibu utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya kilimo hapa nchini kwa kuimarisha huduma za utafiti, upatikanaji na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa visumbufu vya mazao, huduma za ugani, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko.

Waziri Hasunga amesema kuwa Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha inaongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini. Jitihada hizo ni pamoja na Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kukamilisha mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji ili kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia Mipango Shirikishi ya Maendeleo ya Rasilimali za Maji.

Aidha, Wizara ya Kilimo imeendelea kuanisha maeneo ya kipaumbele ya kuongeza tija kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia kwa mazao mbali mbali ukiwemo mpunga.

Amesema, Wizara imeanza na itaendelea kuipitia Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 na sheria mbalimbali kwa lengo la kubaini maeneo ambayo yatapaswa kuhuishwa ili kwenda na hali halisi ya sasa na mwelekeo wa Serikali wa kubadili kilimo chetu kuwa kilimo cha kibiashara. 

Ameongeza kuwa Mtazamo wa Wizara ni kuwa na Sheria moja itakayosimamia rasilimaliwatu, matumizi bora ya pembejeo, ardhi ya kilimo na maeneo mengine muhimu.

Aidha, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali inatambua na kulipongeza Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa-FAO, Serikali ya Venezuela, Halmashauri za Wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero kwa utekelezaji wa mradi wa ubia wa maendeleo ya mifumo ya uzalishaji endelevu wa mpunga Afrika chini ya jangwa la Sahara.

Kwa upande wake Muwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO nchini Tanzania Ndg Fred Kafeero ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuimarisha ushirikiano na Taasisi za kimataifa katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Ameongeza kuwa mradi huo kwa upande wa Tanzania ulilenga kujenga mifumo yenye tija na endelevu katika Afrika ili kuboresha uhakika wa chakula na kuwezesha maendeleo endelevu kupitia mnyororo wa tahamani wa zao la mpunga miongoni mwa wakulima watoto hususani vijana.

Aidha amesema kuwa mradi huo ulilenga kukabiliana na changamoto zinazosababisha uzalishaji mdogo wa mpunga hapa nchini kwa kutambulisha na kusambaza teknolojia ya kilimo shadidi cha mpunga kwa kutumia njia kadhia ambazo FAO imetumia katika nchi nyingine.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Balozi wa Venezuela kwa Kenya na Tanzania Mhe Jesus Manzanilla Puppo, Naibu waziri wa kilimo na Ardhi wa serikali ya Venezuela Mhe Jose Gregorio Aguilers Contreras, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Loata Erasto Olesanare.

MWISHO



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527