JAMBAZI SUGU AFARIKI AKIJARIBU KUWATOROKA POLISI


Mtuhumiwa anayedaiwa kuiba kwa kutumia dawa ya usingizi anayopulizia watu usiku na kuingia ndani mwao, amepoteza maisha baada ya kuruka katika gari la polisi.

Akizungumza na wanahabari jana, Kamanda wa Polisi wa Tarime/Rorya, Henry Mwaibaimbe, alimtaja marehemu ni Boniface John (24) aliyekuwa mkazi wa mtaa wa Bimbwi mjini Tarime.

Alisema alifariki Jumamosi Desemba 21, saa tano wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.

Alisema John alijaribu kuruka katika gari la polisi PT .2016 Toyota Land Cruiser, akiwa njiani kuwaonyesha mahali zilipofichwa mali za wizi.

Alisema aliruka na kuanguka chini na alijeruhiwa sehemu ya nyonga na mguuni, lakini baada ya kufikishwa hospitalini, alifariki wakati akipatiwa matibabu.

Mwaibambe alisema mtuhumiwa huyo alikuwa amebuni mbinu ya wizi kwa kuvunja nyumba usiku baada ya kuwapulizia dawa za usingizi aliowavamia, akifanya hivyo kupitia madirishani na badaye kuingia ndani na kuiba kila kitu alichotaka ikiwa ni pamoja na kuwatoa watu kwenye magodoro waliyokuwa wamelalia na kuwaweka chini.

Aidha, alisema alikuwa akitumia wizi wa silaha pamoja na ubakaji, na baada ya kuhojiwa alikitaja kikosi chake ambacho kinatafutwa.

Alisema alikuwa anatumia dawa hiyo ya usingizi aliyoitoa nchi jirani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post