DK KALEMANI : MARUFUKU NYUMBA ZA TEMBE NA ZILIZOEZEKWA KWA NYASI KUTOWEKWA UMEME

NA SALVATORY NTANDU

Serikali imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi  ya  REA katika maeneo mbalimbali hapa nchini watakaobainika kuzibagua nyumba za tembe na zilizoezekwa kwa majani kwa kukataa kuzipatia nishati ya umeme nyumba hizo licha ya  wamiliki wake kulipia gharama za huduma hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati Dk Medadi Kalemani kwenye ziara ya siku mmoja ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA katika Halmashauri za Ushetu na Msalala mkoani Shinyanga na  kupokea malalamiko ya wananchi kutopatiwa huduma hiyo kwa kigezo cha nyumba zao kutokuwa na ubora.

“Akibainika mkandarasi akifanya ubaguzi kwa wenye nyumba za tembe na nyasi ambao wamelipia gharama za kuunganishiwa umeme serikali haita mvumilia tutamchukulia hatua kali za kisheria”alisema Dk Kalemani.

Katika hatua nyingine DK KALEMANI ametoa siku 30 kwa Mkandarasi Kampuni ya ANGELIQUE INTERNATIONAL.LTD anayetekeleza mradi wa REA katika halmashauri ya Ushetu kuhakikisha anakamilisha kuweka umeme katika vijiji 54 kama mkataba wake unavyoelekeza.

“Kasi yako ya ujenzi wa mradi huu hairidhishi ukishindwa kutimiza ndani ya siku hizo nilizokupa hatua dhidi yako zitachukuliwa hebu ongeza wafanyakazi na vifaa ili kwenda sambamba na masharti ya mkataba wako”aliseme Dk Kalemani.

Fortunata Maila ni mkazi wa Igunda katika Halmashauri ya Ushetu ni miongoni mwa wanufauika na Mradi wa REA awamu ya Tatu amesema tangu huduma hiyo imeanza kutolewa wamenufaika kwa kuanzisha miradi ya ujasiriamali kama vile uzaji wa barafu vinyaji baridi kama vile soda na maji.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha amesema kukamilika kwa mradi wa umeme katika Halmshauri hizo utatoa fursa nyingi za kujiajiri sambamba na kuwataka wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwani imetumia fedha nyingi za serikali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527