BITEKO ALIA NA UPUNGUFU WA MADINI YA CHUMVI VIWANDANI

Na Issa Mtuwa – Dodoma

Upungufu wa madini ya Chumvi kwenye viwanda vya chumvi hapa nchini unamsikitisha waziri wa madini Doto Biteko kutokana na uwepo wa mahitaji (soko) makubwa ya wanunuzi wa madini hayo huku madini hayo yakiwa  hayapatikani kwa wingi kutosheleza mahitaji kutokana na uzalishaji mdogo kutoka kwa wachimbaji wa madini hayo huku wanunuzi wakikosa madini hayo.

Akiongea  tarehe 03/11/2019 ofisi kwake Mtumba jijini Dodoma wakati wa kikao chake na wamiliki wa kampuni wa viwanda vikubwa vya chumvi  hapa nchini Neelkanth Lime anaemiliki; Neelkanth Lime (T) Ltd, Neelkanth Salt(T) Ltd na Rushabh Investment (T) Ltd, Biteko amesema, anasikitishwa na ukosefu mkubwa wa madini hayo huku akiambiwa kuwa kiasi kikubwa cha  chumvi kinachotumika hivi sasa ni kutoka nje ya nchi kutokana uzalishaji mdogo uliopo hapa nchini.

 “Siku zote huwa naumia sana kuona bidhaa au kitu chochote kinacho husiana na sekta yangu (Madini) kikiingizwa kutoka nje wakati uwezo wa upatikanaji wa kitu hicho upo hapa nchini. Kuna wakati tulilazimika kuzui uingizaji wa makaa ya mawe kutoka nje ili kuyapa nguvu masoko ya ndani na leo makaa yam awe yanathamani kubwa. Leo Madini ya Chumvi yanakosekana kwenye viwanda, niseme ukweli naumia sana moyoni.” Alisema Biteko.

Kwa upande wa uongozi wa  Neelkanth Lime (T) wakiongozwa na Ahmed Said Meneja Mkuu akiwa na Rashid Ahmed Mkurugenzi ambao ni wanunuzi wakubwa wa madini ya nchumvi wamesema wanahangaika kupata idadi kubwa ya madini hayo ili kukidhi mahitaji yao hasa kwenye kiwanda chao kilichopo wilayani Mkuranga huku wakiwa wamepandisha bei ya kununua madini hayo hadi Tshs. 160,000/= kwa tani lakini bado mahitaji ni madogo.

“Mhe. Waziri tunahangaika sana kupata haya madini, sisi tumekwenda kila mahali, Lindi, Mtwara na hata hivi majuzi tulikuwa Tanga na tumefanya kikao na wazalishaji wa madini hayo kwenda kuongeza hamasa ya uzalishaji. Nikupe taarifa njema, kuanzia mwezi Februali mwaka huu kiwanda chetu kimeanza kuchakata  tani 1000 kwa siku.” Alisema Rashid Ahmed.

Ahmed, ameongeza kuwa mpaka sasa wastani wa 70% ya chumvi tunayoitumia ni kutoka nje kutokana na upungufu wa uzalishaji wa madini uliopo hapa nchini. Ameongeza kuwa wao wapo teyari kuwaweka wazilishaji wa chumvi kwenye vikundi vidogo vidogo waweze kuunganisha nguvu ili wazalishe kwa wingi huku wakiwawezesha kwa mikopo kama walivyo kufanya huko Mkuranga huku wakimiliki shamba lao la chumvi lenye hekari 2000.

Kutokana na kauli hiyo, kama kawaida Biteko kwa staili ile ile ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli “papo kwa papo” aliinua simu na kumpigia mwenyekiti wa Chama cha Wavunaji Chumvi Tanzania Habib Nour akitaka kuthibitisha kama kweli kuna upungufu wa uzalishaji wa madini ya chumvi na mwenyekiti huyo akapatikana na akamuwekwa “hewani” moja kwa moja mbele ya kikao.

Bila kung’ata maneno, Habib alikiri na kumwambia Waziri kuwa ni kweli kuna upungufu mkubwa wa uzalishaji wa madini ya chumvi hapa nchini huku juhudi za kimkakati wa kuongeza uzalishaji zinaendelea.

Kutokana na hali hiyo Waziri Biteko ametoa wito kwa wachimbaji hasa wadogo kuongeza uzalishaji wao huku akiwasisitiza kukaa kwenye vikundi ili iwe rahisi kupata mikopo kwa ajili ya mtaji ili waweze kuzalisha na kukidhi mahitaji huku  Neelkanth Lime(T) wakisema wako teyari kutekeleza ushauri uliotolewa na Waziri katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa mikopo kweye vikundi vyao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527