WAZIRI MKUU ATOA MAELEKEZO KWA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA AMBAO MAENEO YAO YANA UPUNGUFU WA CHAKULA

Serikali imewaagiza viongozi wa mikoa na wilaya watoe taarifa kama maeneo yao yana upungufu wa chakula na ni kiasi gani kinahitajika.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema jana bungeni mjini Dodoma kuwa, wizara ya Kilimo ikipata taarifa hizo itaratibu vizuri na kuona namna ya kufikisha chakula kwa wananchi kwa kuwauzia ili zipatikane fedha za kununua chakula kingine kiwekwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA).

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Chemba (CCM) Juma Nkamia aliyetaka kauli ya Serikali kwa kuwa baadhi ya mikoa ukiwemo wa Dodoma, Manyara na Singida ina tatizo kubwa la chakula na huenda baadhi ya wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama hawatoi taarifa sahihi kwa sababu ya woga.

“Upungufu wa chakula upo kwa baadhi ya wilaya na maeneo mengine na huu ulitokana na tatizo la hali ya hewa kwamba yapo maeneo msimu uliopita hayakupata mvua ya kutosha. Jambo hili linapotokea kule kwenye ngazi hiyo tunao viongozi…”alisema Waziri Mkuu wakati akijibu maswali ya papo hapo kutoka kwa wabunge wa Bunge la Tanzania.

“Inapotokea kama hali ya hewa imekuwa mbaya Mkuu wa Wilaya akieleza atakuwa anaeleweka kwa sababu pia baada ya kutoa taarifa hiyo timu ya Wizara ya Kilimo itakwenda kuona hali halisi na kuweza kuzungumza na ile mamlaka kuweza kupelekewa chakula kwa bei nafuu” alisema.

Alisema jambo hilo limetolewa ufafanuzi mara nyingi na kwamba, Rais John Magufuli hajazuia kutolewa kwa taarifa za upungufu wa chakula isipokuwa kwenye maeneo yenye hali nzuri ya hewa na kila mmoja ana nafasi ya kulima au kufanya kazi lakini yana upungufu wa chakula.

“Viongozi waliopo kwenye maeneoi hayo wanao wajibu wa kusimamia kila mmoja anafanya kazi pamoja na kulima mazao ya chakula na biashara ili waweze kujipatia tija inapofikia kipindi kama hiki kila mmoja anakuwa na akiba yake” alisema.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara watumie fursa ya tofauti za hali ya hewa kwenye maeneo kuuza chakula sehemu zenye upungufu.

Aliwataka wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa wakutane na wafanyabiashara wawashawishi wapeleke chakula kwenye maeneo yenye upungufu ili kuongeza vipato vyao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527