Serikali imesema inatarajia kuajiri walimu 16,000 wa shule za msingi na sekondari muda wowote kuanzia sasa.
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, alitangaza neema hiyo bungeni jana alipojibu swali la Mbunge wa Mlalo, Abdallah Shangazi (CCM), aliyetaka kufahamu mkakati wa serikali kuhakikisha sekta za elimu na afya zinakuwa na watumishi wengi.
"Sekta za elimu na afya zina upungufu mkubwa sana wa watumishi. Sasa, ni upi mkakati wa serikali kuhakikisha tunapata watumishi wa kutosha kwenda kuwahudumia Watanzania?" mbunge huyo alihoji.
Katika majibu yake, Waziri Mkuu alikiri sekta hizo mbili zina uhitaji wa watumishi kutokana na serikali kutanua huduma zake hadi ngazi ya vitongoji.
“Serikali imeanza kutoa vibali vya ajira katika sekta hizi mbili za afya na elimu, hata kwenye kilimo. Mwaka jana, tuliajiri watumishi 6,000 na sasa tuna kibali ambacho kitatoka hivi karibuni cha watumishi 16,000 kwa upande wa sekondari na msingi.
“Tunaamini baada ya ajira hizi kwenye sekondari na elimu msingi, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa walimu, hivyo hivyo kwenye sekta ya afya, tunataka kuhakikisha tunapeleka wataalamu. Mkakati wa kujenga miundombinu utakwenda sambamba na kuajiri wataalamu," alisema.
Aliongeza kuwa serikali imefanya maboresho makubwa na sera inaeleza kuwa kila kata kuwe na kituo cha afya na kila wilaya iwe na hospitali. Alisema kinachoendelea kwa sasa ni ujenzi wa zahanati na vituo vya afya vyenye uhitaji wa madaktari.