SPIKA NDUGAI ASEMA MBOWE NI MTORO BUNGENI


Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema utoro wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe umekuwa ukisababisha nafasi ya maswali ya moja kwa moja kutoka upinzani kwenda kwa Waziri Mkuu kupotea kila mara.

Ameyasema hayo jana Novemba14,2019  bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu kutoka kwa Wabunge.

Ndugai alisema kwa mujibu wa utaratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola Upinzani hupewa nafasi ya kwanza kuiuliza swali Serikali, lakini kwaa hapa nchini nafasi hiyo hupotea kila wakati kutokana na utoro wa kiongozi huyo.

“Waheshimiwa Wabunge niwataarifu tu kwamba utaratibu wetu wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu swali la kwanza kabisa huwa linakuwa hakiba kwa kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, lakini kwa leo kama mnavyoona kiongozi huyo hayupo,” alisema Spika Ndugai.

Alisema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani anaweza siku zote asiwepo bungeni lakini siku ya Alhamisi ni muhimu awepo kutokana Waziri Mkuu kuwapo na anatakiwa awe wa kwanza kuuliza swali.

“Huwa ni fursa pekee ambayo upinzani wanapata nafasi kwa hiyo kiongozi wa upinzani anaweza asiwepo bungeni siku yoyote lakini siku ya alhamisi ambayo ni ya maswali kwa Waziri Mkuu ni lazima awepo,” alisema Spika Ndugai

Alisema hata hivyo hana taarifa zozote za udhuru kutoka kwa kiongozi huyo (Mbowe) na wala hajui yuko wapi.

“Kwa hiyo hatujapata swali lile kwa kuwa kiongozi wa upinzani bungeni hayupo, uwe wapi, uwe wapi kama Spika hana taarifa zako ni mtoro tu kwa hiyo, ni mtoro na ndiyo maana leo unaona kwamba hiyo fursa ambayo imewekwa kwenye kanuni haijaweza kutekelezwa.

“Na ndio maana mnaona kwamba nafasi inapotea potea sababu ya utoro,”alisema Spika Ndugai.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527