SERIKALI YAWATOA HOFU WANANCHI WA HANDENI MKOANI TANGA


Serikali imewahakikishia wakazi wa Handeni, Mkoani Tanga uendelevu wa huduma ya maji licha ya kuharibika kwa miundombinu ya maji kulikosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa kauli hiyo hapo juzi wilayani hapa wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua athari ya mvua kwenye miundombinu ya maji sambamba na kupata ufumbuzi wa haraka kufuatia hali ya mvua zilizonyesha kwa takribani wiki mbili mfululizo.

Mara baada ya kujionea hali halisi, Mhandisi Sanga aliwatoa hofu wananchi wa Handeni ambapo aliwataka kuwa watulivu na aliahidi kuwa Serikali itahakikisha huduma ya maji inarejea haraka iwezekanavyo.

"Ninawasihi wananchi kufanya subira na kuwa watulivu na kuzingatia maelekezo ya Serikali," alisisitiza Naibu Katibu Mkuu Sanga.

Mhandisi Sanga alibainisha kuwa zoezi la tathmini ya athari ya mvua hizo kwenye miundombinu ya maji wanaloendelea nalo halitochukua zaidi ya siku tatu kama ilivyoagizwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa.

"Waziri wa Maji ametuagiza kuharakisha kukamilisha zoezi hili, nasi tutahakikisha linafanyika kwa kasi ikiwa ni pamoja na kutazama njia mbadala ili wananchi wapate huduma ya maji kwa haraka," alisema Mhandisi Sanga.

Aliongeza kuwa Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli haipo tayari kuona wananchi wake wanataabika na kwamba hatua madhubuti na za haraka zinachukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela akielezea kwa ujumla athari za mvua hizo kwenye Mkoa wa Tanga, alisema kuwa zimeleta madhara kwenye miundombinu ya barabara na madaraja na kusababisha huduma ya usafiri katika maeneo mbalimbali kuathirika.

“Tulichokibaini katika mvua hizi zilizonyesha ni kuwa zimeharibu mabwawa ya maji na kusababisha maji yaliyotoka katika mabwawa hayo kuathiri miundondombinu mbalimbali ikiwemo ya maji na barabara,” alieleza Shigela.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe akielezea athari za mvua hizo alisema ni pamoja na kuharibika kwa mabwawa 11 ya maji yanayotumiwa na wakazi wa Handeni na maeneo jirani na kati ya hayo yapo mabwawa makubwa matano ambayo aliyataja kuwa ni Kwenkambara, Mandera, Suwa, Msomera na Mkomba.

Aidha, Gondwe alipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa wakati na kwa hatua mbalimbali za haraka zinazoendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya barabara na maji iliyoathirika.

Sambamba na hilo, Gondwe alimpongeza Mhandisi Sanga na timu ya wataalam aliyoambatana nayo kutoka Wizara ya Maji na taasisi zake kwa kufika Wilayani hapa mapema ili kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya mabwawa ya maji ili kupata ufumbuzi.

“Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Handeni tunatoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kutujali na kuwatuma watendaji wa Serikali kufika hapa Handeni ili kutatua matatizo yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha,” alisema Gondwe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo ambaye ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Sanga alisema kuwa wanaendelea na tathmini ila kwa mabwawa yaliyopasuka wamebaini yalijengwa chini ya kiwango na pia hayakuwa yakitunzwa inavyostahili na hivyo kupelekea kuharibika wakati mvua hizo zilizonyesha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527