KIJANA ALIYEFUNGWA MINYORORO CHUMBANI AFUNGULIWA SHINYANGA


Kijana wa miaka 26, mkazi wa Old Shinyanga katika Manispaa ya Shinyanga, aliyekuwa amefungwa minyororo chumbani kwa miezi miwili, Shadrack Johanes amefunguliwa na kufanyiwa usafi, kuvishwa nguo na kuanza kupatiwa matibabu ya afya ya akili.


Shadrack Johanes, alifunguliwa minyororo hiyo jana mara baada ya Nipashe kuripoti habari kuhusu ukatili uliokuwa unafanywa dhidi ya na ndugu zake.

Kwa miezi miwili alikuwa amefungwa minyororo mikono na miguu akiwa mtupu huku akila chakula kwenye chumba ambacho alikuwa anajisaidia haja kubwa na ndogo.

Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga, Panuela Samwel, alisema kijana huyo amefunguliwa minyororo hiyo na serikali itatoa matibabu kwake bila malipo.

Panuela Samwel ameongeza kuwa, wameambiwa na wataalamu wa afya kuwa matibabu ya kijana huyo yanatarajiwa kuchukua muda wa miezi sita hadi mwaka mzima. Ofisa huyo wa serikali alisema kama kijana huyo hatapona, watampatia rufani kwenda jijini Dodoma kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mirembe jijini Dodoma.

”Tukio alilofanyiwa kijana huyu ni la kinyama sana, nashukuru vyombo vya habari kwa kuliibua, bila ninyi huenda kijana huyu angefia ndani. Sisi sasa kama serikali, tutamtibu kijana huyu bure kabisa, na leo (jana) anaanza kupatiwa dawa ambayo itachukua muda wa miezi sita hadi mwaka mzima.” amesema Panuela Samwel ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga.

Akiwa kwenye familia ya kijana huyo jana, ofisa huyo aliitaka isimnyanyapae tena, badala yake imweke kwenye mazingira mazuri pasi na kumfunga minyororo.

Mratibu wa Magonjwa ya Afya ya Akili, Brigita Nyangare, alisema kijana huyo hana tatizo kubwa sana la akili kwa kuwa ana bado ana uwezo wa kuongea na hajapoteza kumbukumbu.

Alisema atakuwa karibu na kijana huyo muda wote wa matibabu yake na atakuwa anafuatilia anavyoishi nyumbani hadi pale atakapojiridhisha amepona.

Akizungumza kwa shida, Johanes aliwaomba ndugu zake wasimfungie ndani tena. Ndugu wa kijana hauyo waliomba msamaha kutokana na kumfungia na kuahidi kufuata maagizo waliyopewa na serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527