NAIBU MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI, SISTY NYAHOZA ASEMA WAPINZANI WANATAKIWA KUJILAUMU WENYEWE KWA KUTOFUATA SHERIA ZA UCHAGUZI | MALUNDE 1 BLOG

Sunday, November 10, 2019

NAIBU MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI, SISTY NYAHOZA ASEMA WAPINZANI WANATAKIWA KUJILAUMU WENYEWE KWA KUTOFUATA SHERIA ZA UCHAGUZI

  Malunde       Sunday, November 10, 2019

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza amesema malalamiko yanayotolewa na vyama vya siasa kuhusu kuenguliwa wagombea wao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamesababishwa na wao wenyewe.

Miongoni mwa malalamiko ambayo yalitolewa na vyama hivyo, ni pamoja na wagombea wao kuenguliwa au kuwekewa pingamizi kwa sababu ya kukosa sifa kutokana na kukosea kujaza fomu zao.

Mengine ni wagombea kuenguliwa kwa sababu ya kujaza jina la chama kwa kifupi mfano, Chadema badala ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo au ACT Wazalendo  badala ya Alliance for Change and Transparency.

Nyahoza amesema matatizo na malalamiko mengi yanayovikumba vyama vya upinzani katika uchaguzi huu, yanatokana na kutozingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

“Hivi vyama mara kwa mara tunaongea nao kuhusu kuzingatia sheria na kanuni, sasa kama watakuwa hawazisomi na kuzifuata watakuwa wanalalamika mara kwa mara,” alisema Nyahoza.

Kuhusu fomu inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya mgombea mmoja ambaye amekatwa baada ya kuandika kwa kifupi ACT Wazalendo na kuelezwa na msimamizi wa uchaguzi huo kwamba chama hicho hakipo kwenye orodha ya msajili, alisema chama hicho kimesajiliwa kwa jina la Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) na sio ACT Wazalendo, hivyo hilo ni kosa.

“Hiyo wanayosema ni kifupi ni kama ilivyo CCM kwa Chama Cha Mapinduzi, lakini huwezi kuandika CCM tu kwani inaweza ikawa inamaanisha kitu kingine.

“Sisi kama walezi siku zote tumekuwa tukiwasisitiza kuzisoma na kuzingatia sheria, lakini kama baba unasema na mtoto hafuati matokeo yake ndiyo hayo,” alisema Nyahoza.

Alisema kuwa vyama vyote vya siasa vina wanasheria na watu waliobobea kwenye mambo hayo, ambao wana uwezo wa kuwaongoza wanachama wao katika mambo hayo muhimu.

Credit: Mtanzania


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post