RAIS MAGUFULI ABATILISHA UFUTAJI SHAMBA LA EKARI 1000 MVOMERO

Na Munir Shemweta, WANMM MVOMERO
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amebatilisha pendekezo la kufutwa shamba lenye ukubwa wa ekari 1000 lililopo Kidunda wilayani Mvomero mkoani Morogoro linalomilikiwa na Cecilia George Rusimbi.


Uamuzi wa Dkt Mafuli kubatilisha ufutaji shamba hilo unatokana na kubainika kuwa pendekezo lililowasilishwa la kufutwa shamba hilo kwa madai ya kutoendelezwa kutokuwa za kweli na ulilenga kumdhulumu mmiliki wake.

Akitangaza uamuzi huo wa Raisi jana wilayani Mvomero, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, baada ya kufuatilia mashamba yaliyopendekezwa kufutwa Dkt Magufuli alibaini taarifa alizopelekewa za kufuta shamba Cecilia hazikuwa sahihi na hivyo kuamua kubatilisha pendekezo lililowasilishwa kwake na kumpatia haki yake mmiliki.

Kufuatia hali hiyo Waziri Lukuvi aliwaonya Aaafisa ardhi nchini kuhakikisha wakati wa kufanya zoezi la ukaguzi/Upekuzi wa mashamba yasiyoendelezwa wanazingatia haki pamoja na kufuata sheria badala ya kufanya kazi hiyo kwa upendeleo au kumuonea mtu.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alisema, utendaji kazi katika wilaya ya Mvomero umekuwa wa hovyo na usiozingatia maadili jambo linalopelekea wilaya hiyo kuongoza katika mkoa wa Morogoro kuwa na migogoro mingi ya ardhi sambamba na malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya ofisi ya ardhi.

‘’Baadhi ya watumishi katika ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Mvomero mnajifanya ni Maafisa ardhi au Wapima wakati hamkuajiriwa kwa nafasi hiyo, mnasaini nyaraka za ardhi na kuwaumiza wananchi’’ alisema Lukuvi

Kwa upande wake Cecilia George Rusimbi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kubatilisha ufutaji sahamba lake na kuuelezea uamuzi huo kuwa  umezingatia haki na kusikia kilio chake ambapo alisema umempa faraja baada ya kuhangaika sana kuhusiana na shamba hilo.

‘’ Nimemiliki shamba tangu mwaka 1987 na kuhangaikia hati kwa muda mrefu na nimeshangazwa kuelezwa kuwa shamba langu liko katika mpango wa kufutwa kutokana na kutoendelezwa, hii imenifanya kuishi kwa wasiwasi’’ alisema Cecilia.

Waziri Lukuvi ameagiza shamba hilo la kilimo cha Michikichi, Mitiki na Bamboo  kupangwa upya na mmiliki wake kupatiwa hati kulingana na upimaji utakaofanywa na kumtaka kuliendeleza kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na sakata la shamba la Cecilia, Lukuvi aliagiza kupunguzwa ukubwa wa Shamba Sangasanga na Lubango lililodaiwa kuwa na ukubwa wa ekari 1,103 wakati uhalisia wa shamba hilo ni ekari 500 na kuagiza mmiliki wake kurudisha hati ili apatiwe hati ilinayolingana na uhalisia wake na ekari 603.5 zilizoongezwa zitabaki kuwa ardhi ya akiba.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl Mohamed Utaly alieleza kuwa wilaya yake ina tatizo kubwa la migogoro ya ardhi pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na ofisi yake kukabiliana na tatizo hilo na kuongeza kuwa mingine inachochewa na uhamasishaji unaowafanya wananchi kukata tamaa.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alitembelea ofisi ya Ardhi katika halmashauri ya Mvomero na kubaini ‘madudu’ katika ofisi hiyo ambapo alibaini baadhi ya majalada ya wananchi waliomba kumilikishwa ardhi tangu mwaka 2012 katika halmashauri hiyo kushindwa kupatiwa hati huku.

Hali hiyo ilimfanya Waziri Lukuvi kumuagiza Kaimu Kamishana Msaidizi wa Ardhi Kanda Maalum ya Morogoro Erick Makundi kuhakikisha wale wote walioomba hati na kutumiza vigezo vya kupatiwa hati wanapatiwa kufikia mwezi ujao Desemba 2019. Pia ameagiza kufuatiliwa majalada 300 ambayo wamiliki wake wamekamilisha taratibu za kupatiwa hati lakini hawajapatiwa.

Sambamba na hilo Lukuvi aliagiza wafanyakazi wa ofisi ya ardhi katika halmashauri hiyo wanaojitolea kutosaini nyaraka zozote za ardhi kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakishiriki kutoza tozo kwa gharama za juu za shilingi 50,000 wakati gharama halisi ni 20,000.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527