RAIS MAGUFULI : KUSUSIA UCHAGUZI NAYO NI DEMOKRASIA... AIPONGEZA CCM USHINDI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kitendo cha kususia uchaguzi wa serikali za mitaa huku akikisitiza kuwa maendeleo hayana chama na kwamba Watanzania wanatakiwa kutanguliza mbele maslahi ya taifa. 

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumatano Novemba 27,2019 wakati akizungumza na wananchi wa Isaka wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Rais Magufuli amekipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24,2019.

“Ninapenda kuwashukuru sana ndugu zangu wa Isaka mmemaliza chaguzi, Nimeambiwa Chama Cha Mapinduzi kimepasua vizuri. Hongereni sana,maendeleo ndugu zangu hayana chama na demokrasia hata kujitoa nayo ni demokrasia,kususia uchaguzi nayo ni demokrasia”,amesema Rais Magufuli. 

“Kwa hiyo nawapongeza kwa ushindi mkubwa mlioupata chama cha mapinduzi lakini maendeleo hayana chama ni lazima tushikamane wote kujenga taifa letu,tunachohitaji ni maendeleo,ukileta maji,wote watakunywa,uwe CCM, uwe CHADEMA,ukileta bandari hapa kila mmoja atafanya biashara”,ameongeza Rais Magufuli. 

“Naomba Watanzania tutangulize mbele maslahi ya taifa letu,tuwe wamoja,tujenge Tanzania yetu”,amesema Rais Magufuli.


Hii ni kauli ya kwanza kutolewa na Rais Magufuli tangu baadhi ya vyama vya upinzani kumwomba kuingilia kati madai yao ya wagombea wao kutokutendewa haki wakati wa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita Novemba 24, 2019.

 Baadhi ya Vyama vya Upinzani nchini Tanzania vilisusia uchaguzi wa serikali za mitaa kwa madai ya kutokutendewa haki wakati wa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita Novemba 24, 2019.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527