JAMAA AUA MPENZI WAKE BAADA YA KUMKUMBUSHIA AHADI YA NDOA

Na Asna Kaniki, Mwananchi 

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Paschal (24), anadaiwa kumuua mpenzi wake, Rosemary Gallus (34) mkazi wa Gongo la Mboto kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni na kisha kujiua sababu ikidaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa polisi wilaya ya Ilala, Zuberi Chembela alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita ambapo kijana huyo alikwenda nyumbani kwa Rosemary kwa lengo la kumaliza tofauti zao baada ya kugombana.

“Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja na wamezaa mtoto ambaye ana mwaka na miezi kadhaa, ugomvi wao ulianza baada ya binti kukumbushia kuhusu ahadi yao ya ndoa, mwanaume alisita hivyo binti alianza kutomuamini na ugomvi ukaanzia hapo,” alisema Chembela alipokuwa akizungumza jana kwa njia ya simu.

Hata hivyo baada ya kijana huyo kusita kutoa msimamo wake kuhusu kufunga ndoa binti aliamua kuondoka nyumbani alipokuwa akiishi na mzazi mwenzie na kwenda kupanga Gongo la mboto.

Alisema kwa kuwa marehemu hao walikuwa wazazi, waliendelea kuwasiliana na kijana huyo alipafahamu alipopanga mpenzi wake na hatimaye alikwenda kwa ajili ya kuzungumza na kumaliza tofauti zao.

“Badala ya usuluhishi ikawa ugomvi tena huku mwanaume akimtuhumu mwanamke kuwa anamsaliti kisha kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni mara mbili na kisha yeye mwenyewe kujichoma kitu tumboni mara mbili.”

Alisema kwamba baada ya hapo majirani walisikia mtoto akilia ambapo siyo kawaida yake ndipo walipokwenda kugonga hata hivyo hawakujibiwa, kwa kuwa mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, ndipo baadaye walipoamua kuuvunja mlango huo.

Kamanda Chembela alisema majirani hao walipofika ndani walimkuta mtoto pembeni ya maiti za wazazi wake huku akiwa analia.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Chembela amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kama alivyofanya kijana huyo ambapo alidai kuwa ni kinyume cha sheria.

CHANZO - MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post