RC MWANGELA ATANGAZA KUWACHUKULIA HATUA WAALIMU WATORO NA WACHELEWAJI SHULENI

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akichora mstari wa mahudhurio ya waalimu wa Shule ya Msingi Iyula Wilaya ya Mbozi ikiwa ni saa nne asubuhi mara baada ya kubaini kuwa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo hachori mstari ifikapo saa 1:45 asubuhi ili kuwabaini wachelewaji.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akikagua daftari la mahudhurio ya waalimu wa Shule ya Sekondari Simbega iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na kubaini utoro na uchelewaji wa waalimu katika shule hiyo


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amefanya ziara ya kushtukiza katika baadhi ya shule za Msingi na Sekondari na kisha kumuagiza Afisa Elimu Mkoa kuwachukulia hatua za kinidhamu waalimu wote ambao wanachelewa au kutohudhuria shuleni.
Brig. Jen.  Mwangela ametoa agizo hilo mapema leo mara baada ya kutembelea shule za sekondari za Myovizi na Simbega pamoja na Shule ya Msingi Iyula za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na kubaini utoro na uchelewaji wa waalimu mara baada ya kukagua madaftari ya mahudhurio.
“Mahudhurio ya waalimu sio mazuri, waalimu hawafiki wote katika shule zao na wengine huchelewa sana, pia vitabu vya mahudhurio havijafungwa ifikapo saa moja na nusu na saa moja na dakika 45 kama inavyotakiwa ili kuwabana wachelewaji.”, amesema Brig. Jen.  Mwangela.
Brig. Jen.  Mwangela amesema Afisa Elimu Mkoa anapaswa kusimamia mahudhurio ya waalimu kwakuwa msingi wa taifa unajengwa shuleni na msingi huo hauta imarika endapo waalimu watakosa nidhamu katika kuwahi na kuhudhuria shuleni.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Myovizi Tabu Mtafya amesema amekuwa akitoa onyo kwa waalimu ambao wanachelewa hivyo agizo la Mkuu wa Mkoa ataendelea kulitekeleza.
“Baada ya Mkuu wetu wa Mkoa kukagua kitabu cha Mahudhurio ameniagiza niendelee kusimamia mahudhurio ya waalimu, nami nitawaita waalimu wote wa shule yangu niwakumbushe juu ya kuwahi na kutimiza wajibu wao.”, amesema Mtafya.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo amekiri kuwepo kwa mapungufu ya waalimu kutohudhuria au kuchelewa shuleni na hivyo wamejipanga katika Wilaya ya hiyo kusimamia mahudhurio ya waalimu na kwachukulia hatua za kinidhamu waalimu watoro na wachelewaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527