MUUGUZI ASAKWA KWA KUBAKA HOSPITALINI IGUNGA.... ...'ALIMDUNGA SINDANO YA USINGIZI MREMBO


Baraza la Ukunga na Uuguzi Tanzania, (TNMC)  limeisimamisha kwa muda wa miezi mitatu leseni ya muuguzi, aliyemchoma sindano ya usingizi na kisha kumbaka kuanzia saa nne usiku hadi saa nane msichana mwenye umri wa miaka 16, aliyekuwa akimuuguza mama yake, katika hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Baraza la Ukunga na Uuguzi Tanzania  limeviomba vyombo vya ulinzi na usalama nchini kumkamata popote alipo muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, Damian Mgaya (41) aliyetoroka Hospitalini hapo kufuatia tuhuma za kumbaka binti huyo wa miaka 16 ili afikishwe kwenye vyombo vya Sheria.



Inaelezwa kuwa mara baada ya kumaliza kumbaka binti huyo aliamua kumtupa eneo la kufulia nguo kwenye nyasi akiwa hajitambui na kumwagia maji mwili mzima.


Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 18, 2019, na Msajili wa Baraza hilo Agnes Mtawa na kusema kuwa baada ya mtumishi huyo kurejeshwa kazini, alihamishwa kutoka kituo cha Afya cha Igurubi na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Igunga.

Inaelezwa kuwa muuguzi huyo Damiani Samson Mgaya, mnamo mwaka 2017, akiwa katika kituo cha Afya cha Igurubi , wilayani humo alishawahi kufanya tukio kama hilo, ambapo alipelekwa polisi na kisha mahakamani na hatimae aliachiwa huru na kurejeshwa kazini mwaka 2018.

Kufuatia mtiririko wa matukio hayo kufanywa na muuguzi huyo, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, (TNMC) limeamua kumchukulia hatua ya kusimamisha leseni yake ya kutoa huduma za ukunga na uuguzi popote nchini Tanzania kwa muda wa miezi mitatu.

Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo amethibitisha tuhuma hizo na kusema kesi imefikishwa katika kituo cha polisi.

“Ni kweli tukio lipo na sio mara ya kwanza siku za nyuma Mgaya akiwa kituo cha afya cha Tarafa ya Igurubi alifanya tukio kama hilo, hii ni mara ya pili na huu ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu na kanuni za kiutumishi”- Dkt.Ruta Deus, Mganga Mkuu wa Wilaya.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527